Watu wengi wanachanganya kati ya kaswende na kisonono, haya ni magonjwa mawili tofauti, japo yote ni ya zinaa. Kaswende au syphilis ni ugonjwa sugu unaosababishwa na bakteria wanaoitwa Treponema pallidum. Ugonjwa huu umekuwepo kwa miaka mingi sana, na umekuwa ukitibiwa kwa mda mrefu. Leo tutasoma kwanini upate kaswende sugu na tiba yake.
Kaswende inajificha
Kaswende yaweza kuwa ngumu sana kugundulika, kwani mtu anaweza kuwa nayo pasipo kuonesha dalili zozote kwa miaka mingi. Japo ukweli ni kwamba ugonjwa unapogundulika mapema ndipo nafuu zaidi, kwani utatibikwa na kupunguza hatari ya viungo kuathirika.
Kaswende ikiwepo mda mrefu bila kutibiwa yaweza kuathiri viungo muhimu kama moyo na aubongo.
Utakapoelewa dalili za kaswende, itakusaidia kujilinda na kuwalinda wale uwapendao. sasa twende tuchimbe zaidi kuhusu kaswende, watu gani wapo hatarini na nini cha kufanya endapo umeanza kuugua.
Chanzo Cha Kaswende Sugu
Kaswende inasababishwa na bakteria. Mwaka 1905 mwanasayansi wa kijerumani aligundua kwamba bakteria wa Treponema pallidum wanahusika kuleta kaswende.
Mwanzoni ugonjwa unapoingia, dalili zinakuwa chache sana. Kadiri unavokaa na ugonjwa ndipo maambukizi yanaongezeka na kuathiri maeneo mengi ya mwili.
Kaswende inaambukizwaje?
Njia pekee ambapo bakteria wa kaswende wanaweza kusafiri kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine ni kupitia kwenye majimaji yenye maambukizi. Majimaji haya yanaweza kuwepo kwenye
- mdomo
- uume
- uke na
- mkundu
Kunyonya sehemu za siri inakupa kaswende sugu
Kaswende kwa watu wengi inaambukizwa wakati wa ngono. Kwa maana hiyo siyo tu kufanya tendo, hata unaponyonya uume au uke unapata kaswende. Na wengine hunyonya mpaka mkundu, vyote hivi vinakuweka kwenye hatari ya kuambukizwa kaswende.
Watoto pia wanaweza kuambukizwa kaswende ikiwa mama zao wanaugua. Hii kitaalamu inaitwa congenital syphilis. Pia kaswende yaweza kuambukizwa kwa kuchangia damu.
Imani potofu kuhusu kaswende sugu
Baadhi ya imani potofu ambazo watu wanaamini kuhusu kaswende, imani ambazo siyo kweli na haziwezi kukuambukiza kaswende ni pamoja na
- kushea choo
- kushea nguo
- kutumia vyombo vya kulia chakula
Hii ni kwasbabu bakteria hawa wa kaswende hawawezi kuishi nje ya mwili wa mtu kwa mda mrefu.
Watu gani wapo kwenye hatari zaidi ya kuugua Kaswende?
Kila mtu anaweza kuugua kaswende. Japo kuna baadhi ya makundi yapo kwenye hatari zaidi ya kuugua. Makundi haya ni pamoja na
- watu wenye wapenzi wengi
- wanaofanya ngono pasipo kutumia condom
- wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia mooja
- wagonjwa wa HIV
- watu wenye wapenzi wenye kaswende
Hatua za ugonjwa wa kaswende
Kuna hatua kuu nne za ukuaji wa ugonjwa huu wa kaswende. Hatua hizi ni
- primary(hatua ya awali
- secondary(hatua ya pili)
- hatua ya tatu (latent) na
- hatua ya nne (tertiary)
Kaswende inaambukiza zaidi kwenye hatua mbili za mwanzo. Baada ya hapo kaswende yaweza kuwepo mwilini lakini imejificha bila kuonyesha dalili. Hatua ya nne ni hatari zaidi kwa inaathiri zaidi viungo vya mwili.
Tuanze kuzichambua hatua hizi moja baada ya nyingine ili kama unaugua uweze kujitathmini mwenyewe na kujua upo kundi gani.
Hatua Ya Awali-Primary syphilis
Hatua hii inatokewa kwenye zile week 3 mpaka 4 za mwanzo baada ya kupata maambukizi ya kaswende. Inaanza kwa kupata malengelenge ya mviringo, yasivyouma lakini yanaambukiza. Unaweza hata usijue kama tayari una kaswende, lakini vinaambukiza sana. Vipele hivi vinaweza kutokea popote ambapo bakteria wameingilia kama kwenye mdomo, uume na uke, mkundu na mkundu.
Kwa kawaida malengelenge haya hutokea wiki 3 baada ya kuambukizwa, pia kwa watu wachache inachukua kati ya siku 10 mpaka 90 kujitokeza. Kaswende unaipata unapogusa hayo malengelenge aidha kwenye tendo au kunyonya midomo na sehem za siri.
Hatua ya pili-Secondary syphilis
Kwenye hatua hii unaanza kupata vipele mwilini na koo lako kuanza kuwasha. Kumbuka vipele hivi vinaweza visiume , na vinatokea zaidi kwenye mikono na kwenye miguu. Baadhi ya watu wanaweza wasigundua hivi vipele mpaka vikatoweka.
Dalili zingine kwenye hatua ya pili ya kaswende ni
- kichwa kuuma
- kuvimba mtoki
- homa
- kupungua uzito kuliko kawaida
- nywele kupungua
- kuwasha kwenye joints
Habari njema ni kwamba dalili hizi zitaisha pale utakapoanza tiba. Muhimu ni kutopuuza dalili mbaya kwenye mwili wako. Kwasababu dalili nyingi za kaswende zinafanana na dalili za magonjwa mengine, na ndio maana inatokea hata daktari anachelewa kung’amua kwamba hii yaweza kuwa kaswende.
Hatua ya tatu, kaswende sugu-latent syphilis
Inaitwa latent kwa sababu ugonjwa unajificha kwenye hatua hii. Pamoja na tiba uliyopokea dalili zile tulizoona kwenye hatua ya kwanza na ya pili zitapotea, kujificha kabisa, ila ugonjwa kumbuka bado upo. Hatua hii ya ugonjwa kujificha yaweza kuwepo kwa miaka mingi sana kabla ya kuingia hatua ya nne.
Hatua ya nne-tertiary syphilis
Karibu asilimia 14 mpaka 40 ya wagonjwa wa kaswende wanafikia hatua hii. Na unaweza kuifikia kwa miaka kadhaa au hata miongo kadhaa baada ya kupata maambukizi. Hatua hii ni mbaya zaidi kuliko hatua zote tatu za mwanzo kwani yaweza kuleta madhara kama:-
- upofu
- kupoteza uwezo wa kusikia
- magonjwa ya ubongo
- kuathirika kwa mifupa
- kifafa na homa ya uti wa mgongo
- magonjwa ya moyo
- magonjwa ya neva na uti wa mgongo
Kaswende Sugu inawezaje Kugundulika?
Baada ya kusoma hapa na umeona kwa dalili zako unaweza kuwa na kaswende , nenda hospital mapema sana iwezekanavyo.
Daktari ama muhudumu wa afya atachukua sampuli ya damu na kupeleka maabara kupimwa. Pia daktari atakufanyia uchunguzi kwa kutumia macho kuona kama kuna vipele. Kama una malengelenge, daktari atachukua sampuli ya maji maji kwenye lengelenge na kupima kama lina maambukizi.
Kama daktari atahisi pengine umeshaathirika mfumo wako wa neva, kwasababu ugonjwa umefikia hatua ya nne, anaweza kuuagiza upimwe uti wa mgongo. Hapa watachukua sample kidogo ya majimaji kwenye uti wa mgongo kupima uwezpo wa maambukizi ya kaswende.
Mjamzito Na Kaswende
Kama wewe ni mjamzito unapohudhuria clinic lazima wewe na mpenzi wako mtapimwa magonjwa ya zinaa kwenye hudhurio la kwanza. Unapimwa kwasababu magonjwa ya zinaa yanaongeza hatari ya mimba kuharibika, kuzaa njiti na kuzaa kabla ya wakati.
Kaswende inaweza kuambukiwa kutoka kwa mama mpaka kwa mtoto. Na ndiomaana tiba ya kaswende ni muhimu sana wakati una mimba ili kumlinda mtoto wako.
Kumbuka watoto wanaoambukizwa kaswende kutoka kwa mama wanaweza kupata changamoto za
- kudumaa
- degedege
- homa
- malengelenge
- homa ya majano na
- kupungukiwa damu
Matibabu ya kaswende
Kaswende inapokuwa kwenye hatua ya awali na ya pili yaweza kutibiwa kwa antibiotic ya penicilin. Ikiwa una aleji na penicilin daktari anaweza kukupa dawa zingine kama
doycycline na cefriaxone.
Kama umeshaathirika kwenye neva yani neurosyphilis, utapata dozi kila siku ya penicilin, na utahitaji kulazwa hospitali kwa siku kadhaa. Kumbuka madhara yanayoletwa na bakteria wa kaswende hayawezi kutibiwa ila bakteria mwenyewe anaweza kufa kwa dawa.
Ukiwa kwenye tiba ya kaswende, hakikisha unaacha kufanya ngono mpaka malengelenge yapone na daktari akuruhusu. Ikiwa una mke, au mpenzi wa kudumu , anatakiwa pia yeye apate tiba. Usianze kufanya sex mpaka upone na mpenzi wako atibiwe.
Ufanye nini kujizuia usipate kaswende sugu?
Njia salama kabisa ya kujikinga usipate kaswende ni ngono salama. Tumia condom kila unapokutana na mpenzi mpya na pia hakikisha
- unafanya vipimo mara kwa mara
- kutochangia vifaa vya kupiga punyeto (sex toys), sindano na vifaa ya kujidunga madawa ya kulevya
HIV na Kaswende
Watu wenye kaswende wanaweza kupata ukimwi kwa urahisi zaidi. Hii ni kwasababu yale malengelenge ya kaswende yanaweza kupitisha na virusi vya ukimwi. Na ukumbuke kabisa dalili za HIV zaweza kutofautiana na hizi za kaswende. Ikiwa unahisi dalili tofauti nenda hospitali mapema.
Lini ni mda sahihi wa kupima kaswende?
Hatua mbili za mwanzo za kaswende ni ngumu kugundulika. Dalili za hatua ya pili zinatokea pia kwenye magonjwa mengine, kwahivo unatakiwa kwenda kupima endapo mazingira haya yamejitokeza:-
- umefanya ngono na mtu unayehisi ana kaswende
- una mimba
- unauza mwili(sex worker)
- ni mfungwa gerezani
- umefanya ngono na wapenzi wengi bila condom
- una mpenzi mwenye wapenzi wengi
Kama majibu yakija positive, ni muhimu sana umalize awamu zote za tiba. Hakikisha unamaliza dozi yote na dalili zimepotea. Pia uhakikishe hufanyi kabisa tendo wakati unaendelea na tiba. Upime na ukimwi pia
Ukiugua kaswende ni muhimu kuwajulisha wapenzi wako wote uliokutana nao hivi karibuni, ili wakapime na kutibiwa.
Maswali yanayoulizwa zaidi kuhusu kaswende
1.Je kaswende inaibika asilimia 100?
Jibu ni ndio: Kaswende yaweza kutibuka na kuisha kabisa endapo utaigundua mapema na kumaliza awamu zote za dawa. Japo madhara yoyote ambayo yameshatoea hayawezi kutibiwa na antibiotics
2.Ni dalili gani za awali za kaswende kwenye uume? Lengelenge la kaswende linatokea pale ugonjwa umeingilia, inaweza kuwa uume, uke, mkundu, mapumbu au mdomo. Kadiri ugonjwa unavoelendelea ndipo malengelenge yatajitokeza maeneo mengine ya mwili ikiwemo kwenye mikono
3.Muda gani unaweza kuambukizwa kaswende na usijue: Kaswende isipotibiwa mapema, inaingia kwenye hatua ya tatu ya kujificha yani latency. Kwenye stage hii hutaona dalili zozote. Na virusi vyaweza kujificha ndani ya mwaka mmoja mpaka miaka hata 20. Unaweza kutibiwa hata ukiwa kwenye stage ya ugonjwa kujificha na ukapunguza athari zaidi.
4.Je kipimo kitaacha kusoma positive baada ya kutibiwa?
Kipimo chaweza kuendelea kusoma positive hata baada ya kutibiwa kaswende. Ugonjwa unaweza kuwa umeisha ila kipimo kinasoma positive kwanini? Mwili unaposhambuliwa, kinga inazalisha asktari wanaoitwa antibody, askari hawa ndio hugundulika pale unapopimwa kaswende. Kwahivo waweza kuwa umeshapona kaswende ila askari bado wapo hawajapotea.