Uchafu Mweupe Ukeni Baada Ya Tendo

uchafu mweupe ukeni
uchafu mweupe ukeni

Nini kinasababisha utokwe na uchafu mweupe ukeni kabla na baada ya tendo?
Wakati wa tendo na baada ya tendo kuna majimaji ya rangi nyeupe hutoka ukeni na kwenye uume. Baadhi ya majimaji husaidia tendo lifanyike vizuri na majimaji mengine hutolewa ukeni ili kulinda na kusafisha uke dhidi ya vimelea.

Uchafu Mweupe na Majimaji wakati wa tendo la ndoa

Wakati mwaamke anajiandaa kufanya tendo kutokwa na majimaji ni jambo la kawaida kabisa. Hii ni kutokana na kuongezeka kwa hisia na msisimko wa kimapenzi

Hamu ya tendo na kutomasana au romance kabla ya tendo kunasababisha mzunguko wa damu kwenda kasi na hivo kuleta hisia kali za kimapenzi.

Hisia hizi huleta msisimko mkubwa na kufanya mwanamke akojoe-kwa maana ya kutoa majimaji ya rangi nyeupe. Majimaji haya ni jambo la kawaida kabisa wakati unafanya tendo hivo usiogope.

Mabadiliko ya Homoni kwenye Mzunguko wa Hedhi

Ni jambo la kawaida kubadilika kwa uteute na uchafu unaotoka ukeni kila siku katika mzunguko wako. Mwanzoni mwa hedhi na unapomalizia hedhi ni kawaida kupata uchafu mweupe ukeni na mzito. Wakati wa yai kupevuka ute huwa mweupe mlaini unaovutika kama yai.

Unapokutana na mwanaume kingono katika nyakati hizi ni lazima utaona uteute huu ukitoka, tegemea hilo na usiwe na hofu.

Uchafu Mweupe Ukeni Baada ya Tendo la Ndoa

Kwa kawaida uchafu mweupe baada ya tendo la ndoa ni kiashiria kwamba kuna maambukizi. Maambukizi haya ni

Maambukizi ya Bakteria(Bacterial vaginosis)

Kukua na kumea kwa bakteria wabaya ukeni kunaweza kusababisha utokwe na uchafu mweupe. Pale inapotokea mazingira ya uke yakivurugika kutoka na tendo husika, ama kuosha sana uke mpaka ndani ama matumizi ya sabuni na manukato ukeni.
Uchafu wa maambukizi ya bakteria unaambatana na dalili zingine kama

  • harufu mbaya ukeni kama shombo la samaki
  • uchafu kutoka mwingi kupita kiasi
  • maumivu na muwasho ukeni na
  • maumivu wakati wa kukojoa.

Maambukizi haya ya bakteria yanaweza kutibika hospitali kwa kupatiwa antibiotics. Endapo hutapata tiba mapema ugonjwa unaweza kupelekea changamoto za uzazi kwa siku za baadae.

Maambukizi Ya Fangasi(Yeast Infection)

Fangasi aina ya candida wanapomea kupita kiasi ukeni hupelekea maambukizi ya aina hii. Kwa jina lingine maambukizi haya huitwa vaginal candidias.

Unaweza kupata maambukizi haya kwa ngono na pia pasipo ngono waweza kuugua. Uchafu mweupe ukeni kutokana na fangasi unakuwa mzito, kama maziwa na mara nyingi hauna harufu mbaya.

Dalili zingine ya kuwa una fangasi ukeni ni pamoja na

  • kuhisi kuungua ukeni
  • uke kuwa mwekundu sana
  • maumivu wakati wa kukojoa na
  • maumivu wakati wa tendo la ndoa

Dawa na tiba za fangasi zinapatikana hospitali na kwenye maduka ya dawa.

Magonjwa Ya Zinaa na Uchafu Mweupe Ukeni

Magonjwa ya zinaa yanaweza kupelekea utokwe na uchafu mweupe ukeni baada ya tendo la ndoa. Changamoto hizi huambukizwa kwa njia ya ngono. Magonjwa haya ni pamoja na

  • Chlamydia
  • Trichnomiasis na
  • Gonorrhea

Fahamu tu kwamba magonjwa ya zinaa yanatibika hospitali endapo utawahi mapema kabla tatizo halijawa sugu. Kabla hujashiriki tendo bila kinga hakikisha wewe na mwenzi wako mmepima magonjwa ya zinaa.

Kiwango Gani Cha Uchafu Mweupe Ukeni ni cha Kawaida?

Kila mwanamke anatofautiana namna uke unajisafisha na uwepo wa majimaji. Kujipima jitazame ukiwa hujafanya tendo la ngono, fatilia utokaji wa uchafu na majimaji ukeni katika siku zote za mzunguko wako.

Hapo utaweza kujua ni kiwango gani ni cha kawaida kwako na kipi kinaashiria kuna tatizo.

Tegemea kutokwa na majimaji mengi wakati wa tendo la ndoa. Wanawake kikawaida hupata majimaji na uchafu wa rangi nyeupe wa ujazo wa kijiko kila siku.

Na wanaume kwa upande mwingine hawatokwi na majimaji yoyote isipokuwa wakati wa tendo tu wanapojiandaa kuiingiza uume ukeni na pale wanapofikia mshindo. Kiwango cha kawaida cha mbegu kinajaa kwenye kijiko cha chakula.

Kwa mwanamke kumbuka kama una mamabukizi basi ule uchafu mweupe utaongezeka zaidi wakati wa tendo la ndoa. Ni muhimu kupata tiba na kupna kwanza kabla hujaanza kufanya tendo la ndoa.

Lini Unapaswa Kumwona Daktari

Muone daktari haraka endapo utagundua harufu na mwonekano wa uchafu wako ni tofauti na ulivozoea. Muone daktari endapo uchafu unaambatana na dalili kama

  • maumivu wakati wa tendo
  • mamumivu wakati unakojoa
  • maumivu chini ya kitovu
  • maumivu ya nyonga
  • muwasho sehemu za siri
  • kuhisi hali ya kuungua ukeni na
  • kuvimba uke

Kama huna dalili hizi basi kuwa na amani uchafu wako ni salama kabisa.

Bofya kusoma kuhusu harufu mbaya ya shombo ukeni

3 replies on “Uchafu Mweupe Ukeni Baada Ya Tendo”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *