Kuongezeka uzito Kipindi Cha Hedhi

kuongezeka uzito kipindi cha hedhi
uzito

Je ni kawaida kuongezeka uzito kipindi cha hedhi?

Wakati wa hedhi ni kawaida kuongezeka kilo nne mpaka sita ambazo hupotea baada ya siku chache za hedhi. Ni moja ya dalili za kuelekea hedhi yaani premenstrual syndromes(PMS)
PMS ni mkusanyiko wa dalili zote na mabadiliko yanayompata mwanamke wiki moja kabla ya hedhi. Mabadiliko haya ni pamoja na kuongezeka uzito, uchovu, matiti kuvimba na kuuma, tumbo kujaa gesi na kukosa choo au kupata choo kigumu.

Dalili hizi huletekezwa na mabadiliko ya homoni wakati wa mzunguko wa hedhi. Zaidi wa asilimia 90 ya wanawake wanapata dalili hizi. Sasa tusome zaidi baadhi ya sababu zinazopelekea kuongezeka uzito wakati wa hedhi.

1.Mabadiliko ya homoni

Mabadiliko ya homoni wakati wa hedhi hupelekea mwili kuhifadhi maji mengi na hivo kuongeza uzito. Kuelekea kuanza hedhi yako kiwango cha homoni za estrogen na progesterone hupungua sana na hivo kuutarifu mwili kwamba ni wakati wa ukuta wa mimba kubomoka na kutolewa nje ya uke.

Homoni hizi mbili za estrogen na progesterone ndizo zinaratibu uwezo wa mwili kubakiza maji. Homoni hizi zinapokuwa juu zinafanya tishu za mwili kuhifadhi maji mengi. Mwili unapokuwa na majimaji mengi unafanya viungo kama matiti, tumbo, miguu na mikono kuvimba. Kuvimba huku kunaongeza uzito wako.

2.Tumbo kujaa (bloating)

Bloating ni ile hali ya kuhisi tumbo kujaa na kukaza. Wakati wa hedhi mabadiliko ya homoni yanaweza kupelekea gesi nyingi kujikusanya tumboni na kupelekea tumbo kujaa.

Kujaa huku kwa tumbo na kukaza hupelekea ujihisi kama uzito umeongezeka. Kukaza huku kwa tumbo ni matokeo ya kemikali zinazoitwa prostaglandins, ambazo hutolewa na ukuta wa mimba . Kemikali hizi hufanya ukuta kujikaza na hivo kuvunjikavunjika ili hedhi itoke.

Hali hii ya tumbo kukaza inaweza kuanza siku tano kabla ya hedhi na kuendelea kwa siku chache za mwanzo za hedhi.

3.Ulevi wa vyakula au kula kupita kiasi

Mabadiliko ya homoni kweye kipindi hiki cha hedhi yanaweza kukufanya ukawa mlevi wa kula sana kupita kiwango cha kawaida. Homoni ya serotonin ndio inaratibu mood yako na kiwango cha chakula unachopaswa kula.

Na homoni ya estrogen ndio inayoratibu utolewaji wa serotonin. Kabla ya hedhi estrogen hupungua na hivo kupelekea kiwango cha serotonin kupungua pia, matokeo yake ni wewe kuanza kula kupita kiasi .

Upungufu wa serotonin unakufanya uwe mlevi wa vyakula vya sukari na wanga. Ulaji wa vyakula hivi huongeza uzito kwa haraka.

4.Changamoto za mfumo wa chakula

Mabadiliko ya homoni kwenye mzunguko wako yanaweza kupelekea changamoto kwenye mfumo wa chakula. Changamoto kama kuharisha, kukosa choo na kupata choo kigumu na kiungulia. Kujaa huku kwa tumbo kunaweza kukufanya ujione mzito .

Kiwango cha progesterone huongezeka zaidi wiki moja kabla ya kuanza hedhi. Hii inafanya misuli ya utumbo kuwa legevu na hivo kupunguza kasi ya usagaji wa chakula.

Ni jambo la kawaida kabisa kwa wanawake kupata changamoto za mfumo wa chakula wakati wa hedhi.

5.Upungufu wa madini ya magnesium.

Unapoanza hedhi kiwango cha madini ya magnesium kinapungua mwilini. Kupungua huku kunafanya uwe mlevi wa vyakula na vinywaji vya sukari na hivo kuongezeka uzito ghafla.

6.Kutofanya mazoezi

Wiki moja kuelekea hedhi mwili unaweza kuwa mchovu sana. Jumlisha na zile dalili za tumbo kujaa inakufanya uwe mzembe kufata ratiba yako ya mazoezi. Unapoacha mazoezi kisha ukawa mlaji sana wa sukari na wanga uzito wako utaongezeka maradufu.

Dalili zingine wakati wa hedhi

Ukiacha kuongezeka uzito , unaweza kupata dalili zingine kama

 • Matiti kuwa laini
 • Kukosa choo ama kupata choo kigumu
 • Maumivu ya tumbo na kiuno
 • Kuharisha
 • Maumivu ya kichwa na mgongo
 • Kuota chunusi
 • Hofu na wasiwasi
 • Kukosa usingizi na mwili kuchoka
 • Mood kubadilika na
 • Kukosa hamu ya tendo

Kadiri umri unavoenda dalili unazopata kwenye hedhi zitazidi kubadilika. Zaidi ya asilimia 90 ya wanawake wanapata dalili zaidi ya nne kati ya hizi.

Tiba ya kuongezeka uzito kipindi cha hedhi

Inawezekana kabisa kupunguza majimaji yanayohifadhiwa mwilini wakati wa hedhi kwa kutumia njia za nyumbani(home remedies), na mabadiiliko tu ya mtindo wa maisha na dawa baadhi. Fanya haya

 1. Kunywa maji ya kutosha
 2. Kula chakula cha mafuta mazuri na protini na upunguze wanga na sukari
 3. Unaweza kumeza vidonge vya kupunguza maji mwilili(diuretics) ongea na daktari kwanza kabla ya kutumia vidonge hivi
 4. Tumia virutubishi vyenye magnesium kwa wingi. Hakikisha unashauriana na daktari kabla ya kutumia virutubishi vyovyote.
 5. Fanya mazoezi madogo-tenga walau nusu saa kila siku kuanya mazoezi wakati wa hedhi. Mazoezi yatakusaidia kuchochea usagaji wa chakula tumboni.
 6. Punguza matumzi ya chunvi: Kula chunvi nyingi kunachochea mwili kuhifadhi maji.
 7. Usitumie vyakula vyenye caffeine kwa wingi kama kahawa, energy drinks, chai ya rangi, chocolate na vyakula vinavyozalisha gesi kwa wingi.

Hitimisho

Ni kawaida kuongezeka uzito wa kilo 3 mpaka 5 kipindi cha kukaribia hedhi. Dalili hizi huisha zenyewe baada ya hedhi kuanza. Kupunguza dalili hizi kunywa maji ya kutosha, fanya mazoezi, punguza matumizi ya chunvi na pia punguza vyakula vya sukari na wanga.

Bofya kusoma makala inayofuata: Kuhusu uchafu wa njano baada ya hedhi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *