Fistula

fistula
mwonekano wa fistula

Nini Maana ya Fistula?

Fistula ni neno linalomaanisha muunganiko usio wa kawaida wa viungo viwili vya mwili. Mfano kwa mwanamke kwenye via vya uzazi inatokea sana ukuta unaotenganisha uke na mkundu kutoboka na kupelekea uchafu wa choo na gesi kuvuja mpaka kwenye njia ya uke.

Ajali wakati wa kujifungua kutokana na uchungu pingamizi au upasuaji pia unaweza kuwa chanzo cha fistula. Fistula kwa mwanamke baada ya kujifungua inatibika kabisa, na matibabu yake ni bure hospitali.

Dalili za Fistula ni zipi ?

Kwa fistula ya mwanamke baada ya kujifungua dalili zake ni kama

  • kutoa kinyesi na kijambo kwenye njia ya uke
  • kushindwa kubana haja kubwa kwa muda mrefu
  • kutokwa na harufu mbaya ukeni
  • maumivu wakati wa tendo la ndoa na
  • maumivu katika maeneo yanyozunguka uke

Kama una mojawapo ya dalili hizi ama zote nenda hospitali haraka kwani matibabu ni bure.

Nini Kinasababisha Fistula

Sababu kubwa zinazopelekea mwanamke kupata vistula ni pamoja na

  1. Uzazi pingamizi wakati wa kujifungua: Mwanamke anapopata uchungu kwa mda mrefu pasipo kuzaa, ukuta unaotenganisha uke na mkundu unaweza kuchanika na hivo kukufanya upate fistula.
  2. Ugonjwa wa inflammatory bowel syndrome(IBM):ni changamoto ya kuvimba kwa mfumo wa chakula, inaweza kupelekea upate fistula.
  3. Saratani au tiba ya mionzi kwenye nyonga: Saratani kwenye uke, kizazi au mkunduni inaweza kupelekea fistula. Tiba ya mionzi pia kutibu aina hizi za saratani inaweza kupelekea fistula.
  4. Upasuaji: Upasuaji kwenye uke, mkundu au kwenye utumbo wa mwisho unaweza kusababisha majeraha na hivo kuleta fistula.

Mambo mengine yanayosababisha Fistula ni pamoja na

  • mambukizi kwenye mkundu au eneo la mwisho la utumbo(rectum)
  • kinyesi kuziba kwenye eneo la mwisho la utumbo(fecal impaction)
  • kufanya ngono kinyume na maumbile(maarufu kama kuliwa tigo)

Nani yupo Kwenye Hatari Zaidi ya Kupata Fistula?

Upo kwenye hatari zaidi ya kupata fistula endapo:-

  • umepata uchungu pingamizi(uchungu wa muda mrefu bila kuzaa)
  • ukuta unaotenganisha uke na mkundu ulichanwa wakati wa upasuaji ulipojifungua
  • una magonjwa sugu ya mfumo wa chakula
  • unaugua saratani ya uke, kizazi, mkundu na mlango wa kizazi
  • ulifanyiwa upasuaji wa kuondoa kizazi chote(hysterectomy)

Tafiti Kuhusa Fistula

Tafiti zinasema karibia asilimia 0.5 ya wanawake duniani kote wanaojifungua kwa njia ya kawaida wanapata fistula. Na tatizo ni kubwa zaidi kwa mataifa yaliyoendelea kama Marekani.

Vipimo Hospitali Kugundua uwepo wa Fistula

Kwa wanawake wengi huona aibu sana kuongelea kuhusu fistula. Pamoja na hilo bado kuna umuhimu kumweleza daktari kwa kina ili upatiwe tiba mapema sana.

Daktari atakuuliza kuhusu dalili unazopata na atafanya uchunguzi wake kwa kukutazama eneo husika. Kabla ya daktari kukufanyia upembuzi atavaa kwanza gloves. Daktari anaweza kuamua kuingiza kifaa kinachoitwa speculum ndani ya uke ili kuona vizuri namna ulivopata athari.

Kifaa kingine kinachoitwa proctoscope kinaweza kutumika kumpa daktari picha zaidi ya njia ya haja kubwa na eneo la utumbo wa mwisho.

Matibabu Ya Fistula

Matibabu hasa kwa tatizo la fistula ni madaktari kushona mpasuko au shimo linaroruhusu uchafu wa haja kubwa kuingia ukeni kwa kufanya upasuaji wa muda mfupi.

Endapo utagundulika una mambukizi ya bakteria, daktari atakwanzishia antibiotics kabla ya upasuaji.

Baada ya kukupa dawa za kutibu maambukizi daktari anaweza kupendekeza usubiri miezi mitatu mpaka sita upone kwanza kabla upasuaji. Katika muda huu shimo la fistula linaweza kuziba lenyewe.

Aina za Upasuaji

Upasuji kutibu fistula unaweza kufanyika kupitia njia ya uke, tumbo na kwenye ukuta unaotenganisha uke na mkundu. Wakati wa upasuaji daktari anaweza kuchukua kipande cha nyama kutoka eneo lolote na mwili wako na kuziba tundu la fistula. Upasuaji pia utafanyika kwenye misuli ya mkundu kama imelegea ili kuikaza.

Baadhi ya upasuaji kwa mwanamke mwenye fistula utahitaji kutoboa tundu lingine kwenye tumbo kwa ajili ya kutolea haja kubwa mpaka pale ukipona fistula. Unaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani siku hiyo hiyo baada ya upasuaji kufanyika.

Changamoto gani zaweza kujitokeza baada ya upasuaji?

  • kuvuja damu sana
  • kupata maambukizi ya bakteria kwenye mshono
  • kujeruhiwa kwa viungo vya karibu kama utumbo, mirija ya kibofu na kibofu chenyewe
  • damu kuganda miguuni na kwenye mapafu
  • kuziba kwa njia ya haja kubwa na
  • makovu baada ya upasuaji

Changamoto Anazopata Mgojwa wa Fistula

  • kushindwa kujizuia mkojo na kinyesi
  • kuugua UTI mara kwa mwara
  • kuvimba kwa njia ya uke
  • kutokwa na usaha kwenye tundu la fistula

Nini cha Kufanya wakati Unajiandaa kwa upasuaji?

Wakati unasubiri kwenda kumwona daktari kwa ajili ya matibabu, fanya mambo yafuatayo ili upate nafuu

  1. Tumia dawa za antibiotics kama daktari atakavokwelekeza
  2. Hakikisha unasafisha sehemu za siri vizuri. Osha uke wako taratibu kwa maji ya uvuguvugu endapo utatoa kinyesi ama kujamba.
  3. Tumia wipes zenye unyevunyevu zisizo na marashi au maji masafi badala ya toilet paper unapoenda chooni.
  4. Unaweza kutumia powder ukeni ili kuvyonza unyevunyevu
  5. Vaa nguo za ndani za pamba.
  6. Kama kinyesi kinatoka kila mara bila kujizuia, unaweza kuvaa pedi za watu wazima ili kufyonza uchafu.

Hitimisho

Kwa baadhi ya wagonjwa fistula inaweza kuziba yenyewe bila upasuaji. Mafanikio ya upasuaji kwenda salama unategemea na aina ya upasuaji utakaofanyiwa. Upasuaji kwa njia ya uke na utumbo wa chini unaleta mafanikio karibu asilimia 55. Endapo upasuaji wa mwanzo hautaenda vizuri utafanyiwa upasuaji mwingine.

Kama una ndugu ma rafiki mwenye changamoto hii, mshauri aende hospitali yoyote ya karibu yake haraka kwani matibabu ni bure kabisa.

Bofya kusoma kuhusu: Tendo la ndoa baada ya kujifungua