Mwanamke Kuota ndevu na vinyweleo vingi

mwanamke kuota ndevu
mwanamke mwenye ndevu

Kuwa na vinyweleo kadhaa kwenye kidevu chako kama mwanamke, inaweza kuwa siyo tatizo. Kuna mabadiliko mengi yanaweza kuchangia ikiwemo kuzeeka, homoni na mazingira fulani. Mwanamke kuota ndevu na vinyweleo vingi inaanza kuwa tatizo pale zinapokuwa nyingi sana.

Kitaalamu tatizo la kuwa na vinyweleo vingi maeneo mmbalimbali ya mwili huitwa hirsutism. Ni hali ya mwanamke kuwa na sifa kama za mwanaume. Nyele zinaota kupita kiasi kwenye maeneo ya kidevu, kifua, tumboni na mgongoni. Hali hii inaweza kumuathiri sana mwanamke kisaikolojia, akawa mpweke na kuhisi hana thamani.

Fahamu tu kwamba kuna njia nyingi za asili na rahisi ambazo waweza kufatilia ili kupunguza ndevu na vinyweleo bila kuathirika. Kama wewe ni mwanamke na upo kwenye umri wa kuza (mika 18 mpaka 35) na una ndevu nyingi sana, kuna haja ya kumwona daktari. Unaweza kuwa na tatizo kubwa la kiafya linalopelekea hali yako.

Dalili za kwamba una homoni za kiume zilizozidi

  • kuota nywele nyeusi usoni, kifuani, mgondoni, kwenye mikono, mapaja ama sehemu zingine ambazo siyo kawaida kwa wanawake.
  • chunusi nyingi kupita kiasi
  • kuota kipara
  • matiti kuwa madongo sana
  • misuli kukua na kujaa
  • kisimi kuwa kirefu sana
  • sauti nzito

Nini kinapelekea mwanamke kuota ndevu?

Kila mtu ana vinyweleo kwenye ngozi yake na ni jambo la kawaida kabisa. Kazi ya vinyweleo hivi ni kurekebisha joto la mwili kwa kuruhusu jasho kutoka ama mwili utunze maji.

Wakati wa kubalehe, homoni za kiume(androgens) huongezeka sana na kupelekea vinyweleo hivi kuwa vikubwa mpaka kuwa nywele kamili ambayo ni ndefu na nyeusi. Hii ni kwa wote mwanamke na mwanaume. Wote wana homoni za kike na za kiume ndani yao, ila tu mwanamke ana homoni kidogo za kiume na mwanaume ana homoni kidogo za kike.

Homoni hizi huendelea kubadilika kadiri umri wako unavosogea, unavobadilika uzito, kushika mimba na pia unavokaribia kukoma hedhi. Mabadiliko kidogo tu ya homoni za kiume yanaweza kupekelea uote nywele nyingi mwilini ikiwemo kidevuni. Hapa chini ni baadhi ya changamoto zinazopelekea mabadiliko ya homoni na hatimaye uwe na ndevu nyingi.

Polycystic ovary syndrome(PCOS)

Hii ni moja ya sababu kubwa sana ya kwanini una ndevu kama mwanaume. Kati ya wanawake wanne wenye ndevu basi watatu ni kutokana na PCOS. PCOS inasababisha hedhi kuvurugika na homoni kuvurugika pia na kupelekea uote ndevu nyingi.

PCOS ni tatizo la mifuko ya mayai kushindwa kutoa mayai yaliyopevuka na yanabadilika kuwa vimbe ndogo ndogo nyingi. Pcos linaweza kuwa tatizo la kurithi.

Cushing’s syndrome hupelekea mwanamke kuota ndevu

Hii ni hali ya mwili kuzalisha homoni nyingi ya cortisol. Homoni ya cortisol huzalishwa hasa wakati wa hatari ama ukiwa na msongo wa mawazo ili kuandaa mwili kupambana. Inapozalishwa kila mara inakufanya uanze kuwa na sifa za kiume. Baadhi ya vitu vinavyochangia kuongezeka kwa cortisol ni pamoja na matumizi ya dawa kwa muda mrefu hasa prednisone.

Matatizo ya tezi ya thyroid yanachangia mwanamke kuota ndevu

Pale tezi ya shingoni ya thyroid isipofanya kazi vizuri, inapelekea kupanda ama kushuka kwa uzalishaji wa homoni. Kitendo hiki kinaathiri kazi zingine za mwili. kama una nywele nyingi nenda hospitali kapime homoni ya TSH, T3 na T4 kuona kama kuna tatizo.

Matumizi ya dawa huchangia mwanamke kuota ndevu

Dawa nyingi tu zinaweza kuvuruga mipangilio ya mwili na kukufaya uote ndevu na nywele nyingi kupita kiasi. Pale utakapoenda hospotali kujieleza tatizo, daktari atakuuliza kuhusu dawa unazotumia ikiwemo tiba asili.

Vimbe

Japo inatokea mara chache, lakini vimbe kwenye tezi mfano tezi ya adrenal ama kwenye mifuko ya mayai(ovaries), inachangia uote nywele nyingi kupita kiasi.

Ushauri na njia asili za kurekebisha ndevu na vinyweleo vingi

Naweza kusema wanawake wenye ndevu na vinyweleo vingi na wanahitaji njia asili za kurekebisha tatizo, wana bahati sana. Kwasababu kuna njia nyingi mno za kurekebisha dalili za tatizo. Jaribu kutumia njia hizi za asili na ufatilie mabadiliko kisha utupe mrejesho.

1.Hakikisha uzito wako upo kawaida.

Swala la kurekebisha uzito ni la kwanza endapo unataka kupambana na tatizo na ndevu nyingi, na hasa kama una tatizo la PCOS. Kupunguza uzito itakuepusha pia na changamoto zingine kama kisukari na magonjwa ya moyo.

Fuata hatua hizi kurekebisha uzito wawako

  • Lishe iwe kipaumbele katika kupunguza uzito na mafuta mabaya kwenye mwili. Lishe iwe na vyakula vya kambakamba vingi, protini, na vyakula vyenye mafuta mazuri kama nazi, mafuta ya olive na mafuta ya samaki. na ule chakula siyo zaidi ya mara tatu kwa siku. Unaweza kusoma zaidi kwa kubofya hapa kuhusu lishe ya kupunguza uzito.
  • Epuka baadhi ya vyakula na vinywaji kama vyakula vya ngano, vyakula vyenye mafuta mabaya ya kuhakatwa kiwandani, sukari, vilivyosindikwa kiwandani, vya kwenye makopo, soda na vilivyopikwa kwneye mafuta sana kama chips.
  • Weka ratiba ya kufanya mazoezi: Mazoezi yanasaidia kuchoma mafuta ya ziada kwenye mwili. Jitengee siku 4 za wiki nusu saa kwa siku kufanya mazoezi ya mwili. Mazoezi kama kukimbia, kuruka kamba na kuogelea. Waweza pia kutembea kilomita mbili baada ya chakula cha jioni.
  • Dhibiti msongo wa mawazo: Stress zinakufanya uongezeke uzito na kitambi. Kila siku tenga muda wa kufanya jambo unalolifurahia mfano kusoma vitabu, kuongea na marafiki, yoga, kusikiliza muziki ama kutembea beach.

2.Jali na kuipenda ngozi ya uso wako

Mabadiliko ya homoni yanayopelekea uwe na devu na vinyweleo vingi, pia hufanya uwe na chunusi sana usoni. Chukua hatua hizi kupambana na chunusi

  • Hakikisha uso wako ni safi: Osha uso wako mara mbili kwa siku na siyo zaidi. Tumia kitambaa laini na safi muda wote ama unaweza kutumia vidole kujifanyia scrubing kwa kutumia mafuta asili.
  • Tumia lotion ya asili: Baada ya kuosha uso wako na kukauka unaweza kupakaa lotion isiyo na kemikali kweye uso wako. Hii itafanya ngozi kuwa na unyevunyevu muda wote.
  • Epuka kupaka makeup: Usivae foundation ya usoni wala kupata powder. Vitu hivi hifanya nagozi isipumue vizuri na pia ngozi ya uso kututumka mapema.
  • Usishike ngozi ya uso kila mara: Epuka kubinya chunusi na kushikashika ngozi ya uso kila mara. Hii inapelekea tatizo kuwa baya zaidi na kuharibu ngozi ya uso.

3.Dhibiti hisia zako

Kwa baadhi ya wanawake kuota vinyweleo vingi inaweza kuleta mawazo sana. Endapo unajiona una msongo wa mawazo, unajiona huna thamani kama na huna ule uanamke, inahitaji umuone mtaalamu wa saikolojia. Utahitaji kufanya haya ili kudhibiti msongo wa mawazo na stress

  • Kufanya mazoezi
  • Tafuta mtu wa kuongea nae na kubadilishana mawazo, ongea na wanawake wenzio wenye tatizo kama lako, waulize wanawezaje kuishi na tatizo bila kuathirika akili.
  • Tengenezeza mazingira rafiki ya nyumbani: Mazingira tulivu yatakufanya uwe mtu wa kurelax na kutoawaza sana. Jaribu kutumia mafuta ya lavender yatakusaidia kutuliza akili na usingizi mnono.

4.Weka ratiba nzuri ya kunyoa ndevu na nywele zako.

Pamoja na kwamba umeshapata tiba ya kisasa ama asili kurekebisha dalili zingine kama chunusi,bilshaka una kiu ya kujua namna nzuri ya kuondokana na nywele. Kutoa nywele zilizozidi inaweza kuwa jambo la kukera sana kwa mwanamke. Lakini kadiri unavofurahia njia yako ya kutoa nywele ndivyo zoezi litakavyokuwa rahisi zaidi.

Jaribu njia hizi kama hupendi kuwa na vinyweleo vingi hasa vinavyoonekana mfano ndevu.

  • Nyoa ndevu zako kila siku asubuhi unapoenda kuoga, kama itakulazimu kufanya hivo. Kama ndevu zako zinakua taratibu sana, basi nyoa kila baada ya siku tatu.
  • Jaribu kunyoa kwa mashine za kunyolea, usitumie kiwembe.
  • Unaponyoa nywele, paka kwanza cream laini ya kunyolea, na uwe makini usikwangu chunusi.
  • Nyoa kwa kufaua uelekeo wa nywenye zinapoota
  • Fuata ratiba yako kila mara, ukishajua lini ndevu zinaota na kuonekana.
  • Kama hutapata cream ya kike ya kunyolea, unaweza kujaribu cream ya kiume isiyo na harufu, na ambazo zinafaa kwa ngozi laini.
  • Unaweza pia kutengeneza cream yako nyumbani kwa kuchanganya, mafuta asili ya nazi, mafuta ya lavender, baking soda, mafuta ya olive na vidonge vya vitamin E.

Tahadhari ya kuzingatia

Tatizo la ndevu kwa mwanamke na vinyweleo vingi linaweza kuletekezwa na changamoto kubwa ya kiafya. Muhimu kumwona daktari na kujua kwanza chanzo cha tatizo lako kabla ya kuanza tiba.

Baadhi ya vifaa vya kunyolea, cream, na hata kun’goa nywele vinaweza kusababisha maumivu. Tumia vitu hivyo kulingana na maelekezo ya mtengenezaji, na uache kutumia endapo vinakuletea shida.
Zungumza na daktari endapo dalili zinazidi kuwa mbaya zaidi baada ya kunyoa.

Soma zaidi kuhusu: Michirizi kwenye ngozi na njia salama za kuondoa tatizo

2 replies on “Mwanamke Kuota ndevu na vinyweleo vingi”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *