Maumivu ya kizazi kwa mjamzito

Mimba inapokuwa changa, unaweza kupata dalili za mara kwa mara za maumivu ya kizazi. Unaweza pia kupata dalili za muwasho kwenye uke, chini ya tumbo na kwenye maeneo ya nyonga. Dalili zinaweza kufanana kabisa na zile za kipindi cha hedhi.

Maumivu haya ya kizazi yanaweza kuchochewa na sababu mbalimbali ikiwemo mimba kujipachika kwenye ukuta wa kizazi, kukosa choo na choo kigumu, gesi tumboni na kutanuka kwa kizazi na nyonga ili kumudu kubeba mtoto.

Kama maumivu ni madogo na yanaisha baada ya muda mfupi hapo hakuna cha kuhofia. Lakini kama maumivu ni makali sana, yanachukua muda mrefu kuisha na yanaambatana na kutokwa na damu nyingi ya mabonge, hapo muone daktari haraka.

Soma zaidi kujua chanzo cha maumivu ya kizazi na lini unatakiwa urudi hospitali kupata usaidizi wa haraka.

1.Maumivu ya kizazi kwa Kutanuka mfuko wa mimba

Kwenye wiki za mwanzo za ujauzito wako, unaweza usione mabadiliko yoyote kwenye kizazi. Lakini kuanzia wiki ya 12, kizazi chako kitapanuka na kuanza kukua kufikia size ya chungwa kubwa. Kama una mimba ya mapacha utaanza kuhisi kizazi kutanuka mapema zaidi.

Dalili za kizazi kukua na kutanuka ni pamoja na maumivu chini ya kitovu. Hii ni kawaida kabisa kwa mjamzito na inaashiria kila kitu kinaenda sawa.

2.Gesi au Kukosa choo na choo kigumu

Tumbo kujaa gesi na kukosa choo ni dalili zinatokoea mara kwa mara kwa wajawazito katika miezi mitatu ya mwanzo. Kuongezeka kwa homoni kwa mjamzito zinapelekea kupungua kasi ya usagaji wa chakula. Utapata dalili za choo kuwa kigumu kama cha mbuzi au kukosa choo kwa muda mrefu kuliko kawaida.

Kunywa maji ya kutosha, na kula chakula kidogo kidogo inasaidia kupunguza tatizo gesi na choo kigumu. Kwa kesi ya choo kigumu na kukosa choo, jitahidi kula vyakula vyenye kambakamba kwa wingi, ikiwemo matunda na mboga za majani.

3.Mimba kuharibika

Dalili za mimba kuharibika ni pamoja na

  • kutokwa damu ukeni mfululizo
  • maumivu makali chini ya kitovu
  • maumivu chini ya mgongo
  • maumivu makali ya tumbo
  • kutokwa na mabonge ya damu ukeni

Mjulishe daktari mapema kama unaona dalili hapo juu. Endapo mimba ikishaharibika hakuna namna inaweza kufanyika kunusuru ujauzito. Ni lazima usafishwe na kupatiwa dawa za kuzuia maambukizi

4.Mimba kutunga nje ya kizazi

Ectopic au mimba nje ya kizazi hutokea pale yai lililorutubishwa kujipachika eneo tofauti na kwenye mji wa miba, hasa kwenye mirija ya uzazi. Endapo utapata ectopic basi utajisikia maumivu makali ya kupita kama mshale upande mmoja wa tumbo au kote.

Dalili zingine za mimba kutunga nje ya kizazi ni pamoja na

  • kutokwa na damu nyingi na nzito kuliko hedhi yako
  • kukosa nguvu na kupoteza fahamu
  • changamoto kwenye tumbo la chakula

Mimba ikitunga nje ya kizazi haiwezi kunusurika. Ni lazima ufanyiwe upasuaji ikatolewa haraka ii usipate madhara zaidi.

Matibabu ya maumivu ya kizazi kwa mjamzito

Matibabu kwa maumivu haya yanategemea na chanzo cha tatizo. Maumivu madogo yanayoisha ndani ya muda mfupi hayo hayana shida.

Unaweza kujitibia mwenyewe maumivu ya muda mfupi ukiwa nyumbani kwa kujikanda na maji ya uvuguvugu na kupumzika. Pia unaweza kunywa maji au kitu chochote chenye majimaji. Mweleze daktari kuhusu dalili unazopata anaweza kupendekeza njia nyingine zaidi ya kukusaidia.

Maumivu makali yanayochukua muda mrefu kuisha, yakiambatana na kutokwa na damu au homa yanahitaji usaidizi wa daktari haraka.

Bofya kusoma kuhusu namna ya kulala kwa mjamzito