Kujifungua Kwa Upasuaji

kujifungua kwa upasuaji
mimba

Nini Maana ya Cesarian Delivery?

Kujifungua kwa upasuaji ama cesarian delivery na kwa jina lingine C-section ni upasuaji anaofanyiwa mama mjamzito ili kutoa mtoto tumboni. Upasuaji huu unahusisha kukatwa kwa eneo dogo tumboni na pia kwenye kizazi.

Chanzo Cha kujifungua Kwa Upasuaji

Kikawaida mwanamke anatakiwa kujifungua kwa njia ya uke. Pale mama anapopata matatizo na kushindikana kuzaa kwa njia ya kawaida ndipo inalazimika wahudumu na madaktari kutumia upasuaji ili mtoto azaliwe salama.

Baadhi ya wanawake pia huamua tu kujifungua kwa upasuaji hata kama hakuna ulazima wa kufanyiwa upasuaji ili kulinda njia ya uke isitanuke.

Sababu Kubwa za mjamzito kulazimika kufanyiwa upasuaji ni pamoja na

 • kichwa cha mtoto kuwa kikubwa zaidi na kushindwa kupita ukeni
 • mtoto kutanguliza miguu wakati wa kutoka badala ya kichwa
 • matatizo mengine ya mimba kama kupasuka kwa chupa mapema
 • matatizo ya kiafya kwa mama mjamzito kama presha na kifafa cha mimba
 • mama kuwa na magonjwa ya zinaa ambayo anaweza kumwambukiza mtoto
 • mtoto kutanguliza bega wakati wa kuzaa
 • mtoto kukosa hewa safi ya oxygen
 • matatizo ya kondo la nyuma kama kukatika na
 • historia ya mama kufanyiwa upasuaji kwa mimba iliyopita

Changamoto Zinazojitokeza Baada Ya Kujifungua Kwa Upasuaji

Kuzaa kwa upasuaji ni njia ambayo wanawake wamekuwa wakiipendelea sana kwa miaka ya hivi karibuni. Japo ukweli unabaki pale pale kwamba kuzaa kupitia uke ni njia salama na bora zaidi kiafya. Upasuaji unakuja na changamoto zake lukuki kama

 • kutokwa damu nyingi
 • damu kuganda
 • matatizo ya kupumua kwa mtoto hasa kama alizaliwa chini ya week 39
 • kuongezeka kwa hatari ya kupatwa na changamoto kwenye ujauzito unaokuja
 • kupata maambukizi kwenye kizazi
 • mtoto kujeruhiwa wakati wa upasuaji
 • muda mrefu inachukua kupona ukilinganisha na aliyezaa kikawaida
 • mama kupata majeraha ya upasuaji kwenye viungo vingine
 • hernia/ngiri na matatizo mengine ya tumbo

Muhimu kushauriana na daktari kabla ya kuamua kufanyiwa upasuaji. Daktari kwa kucheki afya yako na ya mtoto atapendekeza kama ni lazima kupasuliwa .

Maandalizi Kabla Ya Kufanyiwa Upasuaji

Endapo wewe na daktari mtashauriana kwamba upasuaji ndio njia sahihi kwako basi daktari atakupa utaratibu mzima ya maandilizi ili kupunguza hatari ya kupata matatizo, na upasuaji ukaenda salama.

Utafanyiwa vipimo mbalimbali kujua grupu lako la damu ili endapo kama utahitajika kuongezewa damu baada ya upasuaji iwe rahisi.

Hatakama huhitaji kuzaa kwa upasuaji ni muhimu kujiandaa kwa hilo kwani yaweza kutokea emergency, yani kulingana na mwenendo wa afya yako pengine ukashindwa kujifungua kawaida na ikatakiwa upasuaji wa haraka ili kuokoa maisha yako na ya mtoto.

Kwasababu kuzaa kwa upasuaji inataka upate muda mrefu zaidi wa kupona, basi ni muhimu ukawa na mtu wa kukusaidia nyumbani hata wawili. Maana kuna baadhi ya kazi hutafanya mpaka pale ukipona kama kufua na kubeba vitu vizito. Wasaidizi wako pia ni muhimu katika kukuogesha na kubembeleza mtoto ili wewe upate muda zaidi wa kupumzika.

Namna Upasuaji Unavyofanyika

Kwanza tenga muda walau siku 3 mpaka 4 za kukaa hospiatali kujiuguza.
Kabla ya upasuaji tumbo lako litasafishwa na utaandaliwa eneo la mkono kwa ajili ya kuchomwa sindano za dawa. Pia utawekewa bomba maalumu(catheter) kuhakikisha kibofu chako hakina mkojo muda wowote.

Utachomwa sindano ya nusu kaputi ili usijitambua kwa muda mpaka pale upasuaji utakapoisha. Baada ya kuandaliwa vizuri na kuchomwa sindano za dawa zote zinazohitajika, daktari atakata kidogo eneo la juu ya mstari wa mavuzi, juu kidogo ya kinena.

Mtoto atatolewa kutoka kwenye kizazi baada ya tundu la pili kukatwa kwenye kizazi.

Daktari atamsafisha mtoto pua zake na mdomo na kukata kitovu. Mtoto atakabidhiwa kwa nesi kuhakikisha kwamba anapumua vizuri kisha baada ya masaa machache utakabidhiwa mtoto wako umshike kwa mara ya kwanza.

Kama uko na uhakika kwamba huhitaji mtoto mwngine tena basi daktari ataweza kukata mirija ya uzazi na kuifunga kabisa siku ile ile.

Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji, Nini Kifanyike

Baada ya upasuaji wewe na mtoto mtakaa hospitali kwa siku 3 mpaka 4. Utaendelea kutumia dawa za kupunguza maumivu pale ganzi itakapopotea.

Baada ya upasuaji daktari atakushauri kupata muda utembee kidogo na kujinyoosha. Hii itasaidia kuzuia damu kuganda na pia kukosa choo. Daktari au nesi atakufundisha namna ya kumbeba mtoto na namna ya kunyonyesha ili usipate maumivu sana kutokana na kidonda.

Daktari atakupa utaribu namna ya kujiuguza ukiwa nyumbani. Lakini muhimu zingatia haya

 • pata muda mwingi wa kupumzika hasa week 4 za mwanzo
 • unapokaa na kulala tumia mkao sahihi kama ulivyoelekezwa ili kupona haraka
 • usifanye tendo la ndoa mpaka week 6 zipite

Soma zaidi hapa hatua za kuzingatia Ili kupona mapema baaada ya upasuaji

One reply on “Kujifungua Kwa Upasuaji”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *