Kipimo cha MRI

kipimo cha MRI
kipimo cha MRI

MRI ni kitu gani?

Kipimo cha MRI kifupi cha magnetic resonance imaging. Kinatumia nguvu ya usumaku (magnetic field) kuzalisha picha nyingi za kiungo cha mwili. Picha ambazo zitamwongoza daktari kujua ugonjwa unaoumwa.

Mwonekano wa kipimo cha MRI

Jinsi kipimo kilivyo ni kama bomba kubwa lenye meza inayotembea, kuruhusu mgonjwa kulala na kuingiwa ndani. MRI inatofautiana na vipimo vya CT scan na X ray kwasababu haitumii mionzi yenye madhara.

Tangu kugunduliwa kwake, kipimo cha MRI kimeshaleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ta tiba. Makala hii itazungumza kwa kina kuhusu MRI, namna kipimo kinafanya kazi na jinis madaktari wanavyokitumia kugundua changamoto za kifya.

Mambo muhimu ya kufahamu kuhusu MRI

 • MRI haileti maumivu wakati wa kipimo
 • Raymond Damadian ndiye aliyetengeneza kipimo cha kwanza cha MRI
 • Gharama ya kunua kipimo cha MRI inaanzia milioni 300 kwa iliyotumika mpaka bilioni 2 kwa MRI mpya.
 • Nchi ya Japan ina machine nyingi zaidi za MRI, machine 48 kwa kila wananchi laki 1.

Matumizi ya kipimo cha MRI

Ugunduzi wa MRI, ni mafanikio makubwa sana kwenye tiba. Madaktari, wanasayansi na hata watafiti sasa wanaweza kutumia MRI kutazama ndani ya mwili wa binadamu kwa kina bila kuleta madhara kwa mgonjwa.

MRI inaweza kutumika katika kutafiti maeneo haya

 • mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye uti wa mgongo na ubongo,
 • kucheki vimbe za saratani na vimbe zenye maji mwilini
 • upimaji wa saratani ya matiti kwa wanawake walio kwenye hatari ya kuugua
 • majereha na chanzo cha maumivu kwenye viungo na mifupa
 • magonjwa ya moyo
 • changamoto za vimbe kwenye kizazi kama fibroids na endometriosis
 • magonjwa ya ini na viungo vingine.

Maandalizi ya kufanyiwa kipimo cha MRI

Kabla ya kipimo, madaktari waakuvisha gauni la hospitali. Daktari atakujulisha kuvua vitu vyote vyenye chuma kama saa, mkufu na pete, vitu hivi zinaweza kuharibu majibu ya vipimo.

Kumbuka hutaweza kufanyiwa MRI, endapo una kifaa cha chuma ndani yako mfano chuma za kufitisha viungo. Pia endapo ulipata ajali, una kifaa cha kurekebisha mapo ya moyo yani pace maker ama risasi mwilini yatakiwa ifahamike kwanza.

vipi naogopa kuingia kwenye mashine ya kupima

Watu wenye hofu na waoga kuingia sehemu zenye utulivu kama bomba kubwa wanatakiwa kumjulisha daktari mapema. Daktari atakupa dawa za kukutuliza kabla ya kuingizwa kwenye kipimo.

Utachomwa sindano yenye kimiminika kwa ajili ya kuimarisha ubora wa picha zitakazotolewa. Kisha wahudumu watakulaza taratibu kwenye kitanda kidogo na kuhakikisha umenyooka vizuri.

Utavalishwa headphone ili uendelee kusikiliza muziki wakati kipimo kinaendelea. Hii inasaidia usipatwe na kelele zinazozalishwa na mashine ya kipimo.

Wakati wa kipimo cha MRI

Ndani ya bomba la mashine ya MRI, mtaalamu wa mionzi ataendelea kuzungumza nawe ili kukuweka sawa tayari kwa kipimo. Mpaka pale utapaokuwa tayari ndipo vipimo vitaanza.

Daktari, mtaalamu wa mionzi aliyebobea kwenye tiba hizi, atazungumza nawe na kukuuliza baadhi ya maswali wakati bado upo ndani ya bomba la kipimo.

Wakati wa kipimo ni muhimu kuendelea kuwa mtulivu bila kusogeza kiungo chochote, itasaidia ubora wa picha. Kuna wakati mpimaji anaweza kukuomba kubana pumzi kidogo. Endapo hujajisikia vizuri kuendelea na kipimo utamjulisha mpimaji ili aache kuendelea na kipimo.

Baada ya kipimo cha MRI

Baada ya kipimo, mtaalamu wa mionzi atafanya upembuzi wa picha zilizozalishwa kuona kama kunahitajika vipimo zaidi. Endapo mtaalamu amejiridhisha, utaruhusiwa kwenda nyumbani kusubiri majibu.

Mtaalamu wa mionzi ataandaa ripoti na kuiwasilisha kwa daktari. Wagonjwa mara nyingi hujulishwa kuweka appointment ya kuonana na daktari ili kusikia kuhusu ripoti na majibu ya vipimo.

Madhara ya MRI

Madhara ya kipimo cha MRI ni madogo sana kama siyo hakuna kabisa.
Japo kabla ya kipimo kuanza, kimiminika kile unachopatiwa kinaweza kuleta kichefuchefu, kichwa kuuma na maumivu eneo ulilochomwa sindano. Pia watu wenye hofu ya kuingizwa sehemu tulivu kama bomba kubwa wanaweza kupata changamoto nyakati za kipimo.

Maswali yanayoulizwa zaidi kuhusu MRI

1.Kipimo cha MRi kinachukua muda gani?

Kufanyiwa scanning kwa MRI huchukua dakika 20 mpaka 60, kwa kutegemeana na eneo la mwili linalofanyiwa upembuzi. Endapo baada ya awamu ya kwanza ya kipimo picha hazina ubora, mpimaji atapendekeza ufanyiwe tena kipimo.

2.Meno yangu yamezibwa, je naweza kufanya MRI?

Japo madini ya mercury yanayotumika kujaza meno yaliyotoboka hayana madhara kwenye upimaji, kwa kiasi kidogo itaathiri ubora wa picha. Daktari na mpimaji watalizungumzia hilo kabla ya kuanza kukupima.

3.Je naweza kufanya MRI nikiwa mjamzito?

Kikawaida madaktari hawapendekezi mjamzito kuchomwa sindano ya kimiminika cha kuongeza ubora wa picha kabla ya kufanyiwa MRI.
Endapo kuna ulazima wa kufanyiwa MRI, itafanyika baada ya muhula wa kwanza wa ujauito.

Soma zaidi kuhusu kipimo cha utrasound hapa