Chanzo cha Mjamzito Kutokwa na Damu

mjamzito kutokwa na damu
mjamzito

Mabadiiko ya mwili kwenye awamu ya kwanza

Katika miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito (first trimester) mwili wako utapitia mabadiliko makubwa sana. Pamoja na kwamba utaendelea kuvaa nguo zako zile zile na zikakufiti lakini ndani ya mwili kuna mabadiliko mengi yanafanyika.

Hii ni pamoja na kuongezeka kwa homoni na pia utengenezaji wa mzunguko mpya wa damu kwa mtoto. Mabadiliko haya yanaweza kupelekea mjamzito kutokwa na damu nyepesi ukeni.

Tafiti zinasema kwamba asilimia 30 ya wanawake wote wajawazito hutokwa na damu nyepesi katika miezi mitatu ya ujauzito wao. Hili ni jambo la kawaida kabisa. Wanawake wengi hupata bleed nyepesi na wanajifungua vizuri kabisa.

Kuna sababu nyingi zinazochangia utokwe na damu. Tuzisome kwa kina hapa chini.

Mjamzito kutokwa na damu miezi 3 ya kwanza

Kupata matone ya damu siyo jambo la kupata hofu, hasa kama itaisha ndani ya siku mbili. Kwa upande mwingine kama utaendelea kubleed damu nyingi zaidi ya siku mbili unatakiwa kuwahi hospitali kwani ni kiashiria cha mimba kutishia kutoka.

Kutokwa damu baada ya yai kujipachika kwenye kizazi

Kitaalamu inaitwa implantation. Ni kitendo cha yai lililorutubishwa kuchimba na kujishikiza kwenye ukuta wa kizazi. Mchakato huu unatokea katika siku ya 6 mpaka 12 tangu uliposhika mimba.

Yai lililorutubishwa ni lazima kujishikiza kwenye ukuta wa mji wa mimba ili kupata huduma muhimu kama hewa safi na lishe.

Kitendo hichi chaweza kupelekea utokwe na matone kidogo ya damu. Matone haya ya damu utayaona kabla ya tarehe yako ya kupata hedhi . Wanawake wengi huchanganya bleed hii ya mimba na ile ya hedhi.

Je ni damu ya hedhi au bleed ya mimba?

Kutofautisha kati ya bleed ya mimba na ile ya hedhi ni ngumu sana. Kwasababu dalili nyingi zinazoambatana zinafanana.

Dalili kama

  • kichefuchefu
  • maumivu chini ya mgongo
  • maumivu kiasi ya tumbo
  • matiti kuwa laini

Dalili kubwa inayotofautisha bleed ya hedhi na ile ya mimba ni kwamba, bleed ya mimba inakuwa nyepesi sana na rangi isiyokolea na inapotea mapema ndani ya masaa kadhaa.

Uvimbe kwenye mlango wa kizazi (cervical polyp)

Karibu asilimia 2 mpaka 5 ya wanawake hupata uvimbe huu, uvimbe unakuwa mdogo kama kidole kwenye mlango wa kizazi. Uvimbe huu mara nyingi siyo wa saratani/ japo kuna wakati waweza kuongezeka na kupelekea utokwe na damu nyepesi.

Mjamzito kutokwa na damu baada ya tendo

Kwa mwanamke kitu chochote ambacho kinaingia ukeni kinaweza kusababisha majeraha na kutokwa na damu. Iwe ni uume wakati wa tendo la ndoa au kifaa cha vipimo kinachoingizwa kwa njia ya uke. Ukipatwa na hali hii usipaniki ni hali ya kawaida na itapotea baada ya muda mfupi.

Mimba kuharibika

Kwa mjamizito kutokwa na na damu nyepesi inaweza kugeuka uwa mabonge ya damu nzito. Ni kweli kwamba kutokwa na damu nyingi na nzito kwa mimba ya chini ya miezi mitatu huku ikiambatana na maumivu makali ya tumbo ni ishara ya mimba kuharibika.

Mimba nyingi huwa zinaharibika katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo. Kama mimba yako inatishia kutoka, utapata dalili kama

  • kutokwa damu nyingi ukeni
  • maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu
  • mumivu chini ya mgongo
  • kutokwa na mabonge ya damu iliyoganda

Kama unapata dalili hizi hakikisha unaenda hospitali mapema kuonana na daktari. Endapo utawahi hospitali unaweza kupata huduma na mimba ikabaki salama. Sababu za mimba kutishia kutoka ni pamoja na maambukizi kwenye kizazi, matumizi ya baadhi ya dawa na kizazi kulegea.

Mjamzito kutokwa na damu kutokana na mimba ya mapacha

Kama umebeba mimba ya mapacha kuna uwezekano mkubwa zaidi ukatokwa na damu nyepesi. Mimba nyingi pia zinaharibika kwa wajawazito wenye mapacha.

Mimba kutunga nje ya kizazi

Ectopic au mimba kutunga nje ya kizazi inatokea pale yai lililorutubishwa kujishikiza eneo lingine tofauti na kwenye mji wa mimba. Mimba za namna hii nyingi hutokea kwenye mirija ya uzazi. Mimba inapotunga kwenye mirija haiwezi kukua. Dalili za mimba nje ya kizazi ni pamoja na

  • kutokwa damu nyepesi
  • maumivu ya haraka
  • maumivu makali ya tumbo na
  • kuhisi mgandamizo eneo la haja kubwa

Endapo una dalili hizi, fahamu kwamba hujakosea popote, na mimba hii haiwezi kukua inatakiwa iondolewe kwa upasuaji mapema.

Molar preganancy

Chanzo kingine cha kutokwa damu kwa mjamzito ni aina hii ya mimba-molar pregnancy. Inatokea mara chache sana lakini ni tatizo kubwa linalohitaji matibabu haraka.

Ni aina ya mimba ambapo kondo la nyuma linalotumika kusafirisha lishe na hewa kwenda kwa mtoto kukua kupita kiasi. Ukuaji huu huchangiwa na mabadiliko ya vinasaba wakati wa urutubishaji. Mtoto anaweza asikue kabisa. Molar preganancy inaweza kusababisha mimba kutoka ndani ya miezi mitatu ya mwanzo.

Mjamzito kutokwa na damu kutokana na maambukizi

Maambukizi kwenye njia ya mkojo(UTI) na kwenye njia ya uzazi(PID) yanaweza kupelekea utokwe na damu. Maambukizi haya yanaweza kusababishwa na bakteria, fangasi au virusi. Ukiwa na maambukizi utapata dalili hizi

  • muwasho ukeni
  • maumivu chini ya kitovu
  • maumivu makali wakati wa kukojoa
  • kutokwa na uchafu mwingi mweupe
  • vipele au malengelenge kwenye mashavu ya uke

Kutokwa na damu miezi 6 mpaka 9 ya ujauzito

Kutokwa damu kipindi hichi cha mimba kubwa ni hatari zaidi ukilinganisha na pale mimba ikiwa changa. Chanzo cha tatizo ni pamoja na

  • matatizo kwenye mlango wa kizazi
  • kukatika kwa kondo la nyuma kabla ya muda wa leba (placenta abruption)
  • kondo la nyuma kuziba mlango wa kizazi (placenta previa)
  • uchungu wa mapema kabla ya muda sahihi wa kujifungua(premature labour)

Lini Unatakiwa Kumwona Daktari

Muone daktari endapo unapata dalili zozote za kutokwa damu wakati wa ujauzito. Hakikisha unapata uangalizi mkubwa endapo utaona dalili hizi

  • kutokwa damu nyingi na nzito
  • kutokwa damu iliyoganda
  • maumivu makali
  • kukosa nguvu na kuanguka
  • joto kupanda na homa kali

Tiba ya hospitali kwa mjamzito anayetokwa damu ukeni

Baadhi ya vyanzo vya tatizo kama uvimbe kwenye mlango wa kizazi zinaweza kutibiwa haraka. Baadhi ya changamoto zitahitaji matibabu makubwa, dawa na hata upasuaji.

Kama bleed yako inatishia mimba kuharibika, daktari anaweza kukupa dawa kama

  1. Methotrexate: dawa inayofonza tishu zisizo salama kama tishu za ectopic
  2. Misoprostol: inatumika kutoa mimba ya chini ya wiki saba.

Baada ya tiba utahitaji kuendelea kuhudhuria clinic kwa siku kadhaa mpaka upone. Daktari atakufanyia vipimo mara kwa mara kuona kama hakuna mabaki ya mimba kwenye kizazi baada ya mimba kutoka.

Daktari pia atakushauri ni baada ya muda gani itakuwa salama kushika ujauzito mwingine.

Unahitaji maoni ama ushauri? Tuandikie kwa whatsapp namba 0678626254 utajibiwa, Usipige simu namba ni ya whatsapp tu.

Soma makala inayofuata kuhusu: Njia salama za Kusafisha kizazi baada ya mimba kuharibika

3 replies on “Chanzo cha Mjamzito Kutokwa na Damu”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *