Je inachukua Muda gani Kushika mimba?

ufatiliaji wa mzunguko-kushika mimba
mzunguko

Kwa baadhi ya wanawake kushika mimba yaweza kuchukua muda mrefu zaid kuliko ilivotegemewa. Kwa wengi kushika mimba ni kitendo cha kugusa tu bila hata kutumia nguvu nyingi.

Ni muhimu sana kulinda afya yako pale unapojiandaa kushika ujauzito. Acha kutumia pombe, kuvuta sigara na madawa mengine ya kulevya. Anza pia kutumia baadhi ya vitamins za kuboresha afya yako kuandaa kubeba ujauzito

Uwezo wa kushika mimba unatofautiana

Usijilinganishe na wanawake wenzako maana mnatofautiana pakubwa. Baadhi ya vitu muhimu ambavyo vinachangia uwezo wako wa kushika mimba mapema kama

 • umri wako
 • afya yako kwa ujumla
 • historia ya familia yako na
 • mara nyingi kiasi gani unakutana na mwenzi wako kingono.

Wapenzi wengi hufanikisha suala la ujauzito katika muda wa miezi 6 mpaka mwaka mmoja. Kama umetafuta ujauzito kwa mwaka mzima na hujafanikiwa jaribu kumwona mtaalamu wa magonjwa ya uzazi kupata ushauri na tiba.

Mara nyingi chanzo cha kukosa mimba kinaweza kugundulika na kutibika hospitali, lakini kwa kesi chache sana chanzo cha kukosa ujauzito kinaweza kisigundulike kabisa pamoja na kufanyiwa vipimo vyote.

Inachukua Muda gani kwa Mwanamke Kushika Mimba?

Wanawake wengi wana uwezekano mkubwa kushika mimba katika miaka ya ishirini. Hapa ndipo unakuwa na hifadhi kubwa ya mayai. Uwezo wa kushika mimba huendelea kupungua kadiri umri unavokwenda.

Kadiri unavozeeka ndipo uwezo wa kushika ujauzito unapungua zaidi.
Unapofika miaka 35 unakuwa na chansi ya asilimia 12 tu kushika mimba. Ukifika miaka 40 chansi inapungua zaidi mpaka asilimia 7.

Uwezo wa mwanaume pia kumpa mimba mwanamke unapungua kadiri umri unavoenda. Mbegu za mwanaume mzee zinakuwa na hitilafu zaidi.

Nini Kinasababisha Ugumba Kwa Mwanamke?

Ugumba kwa wanawake inachangia kwa asilimia 30 ya kesi zote za kukosa mimba. Tatizo kubwa likiwa kwenye mayai kupevuka. Kama yai lisipopevuka haliwezi kutolewa kwenye mfuko wa mayai ili likarutubishwe. Mayai yanaweza kutopevuka kutokana na changamoto mbalimbali kama

 • Polycystic ovarian syndrome(PCOS)-Vimbe kwenye mayai.
 • Premature ovarian insufficiency(POI)-mifuko wa mayai kushindwa kuzalisha mayai katika umri mdogo chini ya miaka 35.
 • Kuziba kwa mirija pia ni chanzo kikubwa cha mbegu kushindwa kulifikia yai. Sababu kubwa za kuziba huku ni pamoja na
 • Maambukizi kwenye kizazi(PID)
 • Kizazi kupanuka(endometrosis) na
 • Historia ya upasuaji kwa ajili ya mimba iliyotunga nje ya kizazi(ectopic).
 • Matatizo kwenye kizazi pia yanaweza kukufanya ushindwe kushika ujauzito. Hii inaweza kuwa kutokana na maumbile yasiyo ya kawaida au pengine kukua kwa vimbe(fibroids)

Nini Kinasababisha Ugumba kwa Wanaume?

Ugumba kwa wanaume inachangia karibu asilimia 8 kwa wapenzi kukosa mtoto. Sababu kubwa ikiwa ni pamoja na

 • kuvimba kwa mishipa midogo ya damu kwenye mapumbu(varicocele)
 • mbegu kuwa na maumbile yasiyo ya kawaida
 • majeraha kwenye korodani yanayopelekea kupungua uzalishaji wa mbegu
 • kunywa pombe kupita kiasi na uvutaji sigara
 • tiba ya mionzi na chemotherapy
 • changamoto za tezi zinazohusika na uzalishaji wa mbegu
 • matatizo ya vinasaba kwa kesi chache sana

Tiba ya Ugumba

Wataalamu wa magonjwa ya uzazi hutoa tiba mbalimbali kwa kulingana na aina ya tatizo. Aina ya tiba ambayo daktari atakupatia inategemea na umri wako, afya yako na chanzo chako cha ugumba.

Daktari anaweza kuamua kukupa dawa za kumeza kwa mwanamke kuchochea mayai kupevuka. Na kwa mwanaume dawa utapewa za kuongeza uzalishaji wa mbegu.
Endapo itatokea dawa hazijasaidia daktari anaweza kupendekeza mwanamke ufanye upasuaji mdogo kuzibua mirija endapo una tatizo hili. Ama akapendekeza kupandikiza mimba kama njia zote zingine zimegonga mwamba.

Bofya kusoma makala inayofuata kuhusu: Hatua za kupandikiza mimba

3 replies on “Je inachukua Muda gani Kushika mimba?”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *