Nini maana ya mlango wa kizazi
Mlango wa kizazi ama shingo ya kizazi ni mlango kati ya uke na kizazi(uterus). Ni eneo la chini ya kizazi na juu ya uke wako lenye mwonekano kama donati. Makala yetu itachambua kwa kina tatizo la mlango wa kizazi kufunga na nini cha kufanya.
Mlango wa kizazi ni kama kipa golini, kufatilia kila kinachotakiwa na kichotakiwa kuingia kwenye kizazi.
Kuziba na kufunguka kwa mlango wa kizazi
Ukiwa hauna mimba na upo kwenye siku za kawaida, siyo za hatari, mlango wa kizazi unazalisha uteute mzito unaoziba kwenye mlango. Ute huu mzito unapoziba unazuia mbegu kuongelea na kupenya kwenye kizazi.
Unapoingia kwenye ovulation ama siku za hatari, mlango wa kizazi unazalisha uteute mlaini kama yai. Hapa mlango wa kizazi utakuwa pia mlaini sana kuliko siku zingine za mzunguko. Kazi ya ute huu wa yai ni kusaidia mbegu kuogelea na kupenya kwenda kurutubisha yai.
Kuelekea hedhi mlango unakaribia kufunga na Kisha Kufunguka tena
Siku chache kuelekea kwenye hedhi, shingo ya kizazi inakuwa ngumu na kubadilika mkao. Mlango wa kizazi unapungua na kujiandaa kuziba endapo mimba imetungwa.
Kama hakuna mimba shingo ya kizazi inalegea na mlango kuachia ili kuruhusu damu kutolewa kupitia njia ya uke.
Nyakati zingine mlango wa kizazi unaweza kufunga wakati unatakiwa kuwa wazi. Changamoto hii kitaalamu inaitwa cervical stenosis. Baadhi ya wanawake wanazaliwa na hali hii na wengine wanaipata baadae kwenye maisha.
Dalili za mlango wa kizazi kufunga
Ukiwa na tatizo la kufunga mlango wa kizazi, utapata maumivu makali kwenye hedhi ama chango. Lakini hili siyo tatizo pekee linapelekea chango la uzazi, ndiomaana ni muhimu kwenda hospitali kupata vipimo.
Kizazi kilichofunga kinapelekea ushindwe kushika mimba kwasababu ya kuzuia mbegu kuogelea kuingia kwenye kizazi.
Na endapo tayari umeshakoma hedhi, waweza usione viashiria vyote.
Nini kinachopelekea mlango wa kizazi kufunga?
Vitu vinavyosababisha mlango wa kizazi ufunge wakati ambao unatakiwa kuwa wazi ni pamoja na
- Upasuaji kwenye kizazi
- Kukatwa nyama za mlango wa kizazi kwa ajili ya vipimo(cone biopsy)
- Tiba ya saratani kwenye mlango wa kizazi
- Vimbe kwenye mlango wa kizazi
- Tiba ya mionzi
- Endometriosis na
- Makovu kwenye mlango wa kizazi
Vipimo kugundua kama kizazi kimefunga
Kujua kama una tatizo la mlango wa kizazi kufunga, daktari atakufanyia vipimo kwenye via vya uzazi. Kipimo cha kwanza ni kuingia kifaa kwenye uke, ili kuona shingo ya kizazi. Hapo atacheki rangi na size. Pia atangalia kama kuna uwepo wa vimbe ama uchafu wowote usio wa kawaida
Matibabu ya Kufunga mlango wa kizazi
Matibabu ya kuziba mlango wa kizazi inategemea na sababu nyingi ikiwemo
- umri wako
- endapo unahitaji kuzaa
- dalili unazopata kwa muda huo
Kama huhitaji kushika mimba, na hauna dalili zozote mbaya, basi huhitaji kabisa tiba.
Lakini kama unatafuta mimba bila mafanikio, na unapata maumivu makali kwenye hedhi na tendo la ndoa, itahitaji upate tiba ya kupanua mlango wa kizazi.
Je kizazi kilichofunga kitaniletea matatizo zaidi?
Endapo mlango wa kizazi umefunga ama kusinyaa, unaweza kupata changamoto kama
- kushindwa kushika mimba
- hedhi kuvurugika
- maumivu makali kwenye hedhi
- maji kujikusanya kwenye kizazi na
- usaha eneo la mlango wa kizazi