Changamoto ya mjamzito kutapika na kichefuchefu ni dalili za kawaida za mimba. Kwa lugha ya kitabibu huitwa morning sickness, inaweza kukufanya ukose raha na kushindwa kula vizuri.
Kutapika na kichefuchefu inatokea hasa miezi mine ya mwanzo na ni dalili kuu ya kwanza kukuonesha tayari una mimba. Usihofu chochote, fahamu tu kwamba hakuna madhara wa ujauzito na kuna vitu kadhaa unaweza kufanya kupunguza makali ya tatizo.
Chanzo cha mjamzito kutapika na kichefuchefu.
Hakuna chanzo kimoja kwa dalili hizi kwa mjamzito, na makali yake yanatofautiana kwa kila mwanamke. Kuongezeka kwa homoni katika wiki za kwanza za ujauzito ni chanzo kikubwa cha kutapika na kupatwa na kichefuchefu. Pia kupungua kwa sukari kwenye damu ni chanzo kingine cha morning sickness.
Sababu zingine zinazoongeza makali ya kichefuchefu na kutapika ni pamoja na
- Mimba ya mapacha
- Msongo wa mawazo
- Uchovu kupita kiasi
- Kusafiri kila mara
Dalili hizi zinaweza kuwa tofauti kwa kila ujauzito. Mimba ya kwanza inaweza kukupeleksha sana lakini mimba zinazofuata kutapika na kichefuchefu kikapungua kwa kiasi kikubwa.
Madhara madogo ya mjamzito kutapika na kichefuchefu
Kutapika na kichefuchefu kinaweza kupelekea kupungua kwa hamu ya kula. Wanawake wengi hupata hofu sana kwamba hali hii yaweza kumdhuru mtoto. Usiwe na hofu dalili hizi hazina madhara kwa kiumbe cha tumboni.
Japo wanawake wanaopata kichefuchefu na kutapika kwa mimba ya zaidi ya 3 mpaka 4 wanatakiwa kwenda hospitali kumwona daktari. Pia muone daktari endapo una mimba lakini hujaongezeka uzito kabisa.
Kichefuchefu na kutapika siyo matatizo makubwa kiasi ya kuzuia ukuaji wa mtoto. Kwa baadhi ya wanawake kichefuchefu huwafanya kutapika kupita kiasi mpaka kupungua uzito.
Lini unatakiwa kumwona daktari?
Nenda hospitali haraka endapo utapata dalili hizi
- kutapika kila unapokula
- kupungua kilo tatu na zaidi
- homa
- kukojoa mara kwa mara mkojo mweusi
- kuhisi kizunguzungu
- kutapika damu
- maumivu ya kichwa mara kwa mara
- maumivu makali ya tumboni
- kutokwa na damu ukeni
Tiba/ vyakula na virutubisho kupunguza makali ya kichefuchefu
Baadhi ya wanawake hupata nafuu ya kupungua kichefuchefu na kutapika kwa kutumia vitu hivi. Muhimu mjulishe daktari wao akupe ushauri kama ni salama kuvitumia kulingana na hali yako.
- Virutubishi vya vitamin B-6
- Multivitamins
- Tangawizi
- Barafu na
- Maembe mabichi
Vipimo kwa tatizo la mjamzito kutapika na kichefuchefu
Kwa kulingana na ukubwa wa dalili zako, daktari anaweza kuagiza ufanyiwe vipimo hivi kuona kama mimba iko salama. Vipimo hivi ni pamoja na
- Kipimo cha mkojo: Kucheki kama una upungufu wa maji.
- Kipimo cha damu: kucheki kama una damu ya kutosha na kama kuna upungufu wa vitamins
- Utrasound: Kucheki kama mtoto anakua vizuri tumboni
Ushauri mwingine ili kupunguza morning sickness
Ukifuatilia hatua hizi zitakusaidia kupunguza ukubwa wa tatizo
- kunywa maji ya kutosha kila siku
- kunywa maji kabla na baada ya kula
- pumzika mara kwa mara
- hakikisha sehemu unapokaa au kufanya kazi kuna hewa ya kutosha
- epuka vyakula vinavyoamsha mwili kama pilipili
- punguza vyakula vya mafuta
- meza vidonge vya vitamin jioni
- epuka moshi wa sigara
Kama hatua zote hizi hazitakupa matokeo, au kama unapata kichefuchefu na kutapika mpaka miezi 3 au mi4 ya mimba, ni muhimu uende hospitali. Pia hakikisha unapata ushauri wa daktari kabla ya kuanza kutimia dawa au virutubishi vyovyote ikiwemo tiba asili.