Nini Maana ya kupandikiza Mimba(IVF)?
IVF ni kifupi cha maneno invitro fertilization. Ni mojawapo ya teknolojia ya kusaidia mwanamke kupandikiza mimba, Endapo njia ya kawaida ya uke na uume kukutana vimeshindikana kutokana na sababu mbalimbali za kiafya.
IVF inajumuisha kuchukuliwa kwa yai lililopevuka kutoka kwenye mfuko wa mayai na kisha yai hili kurutubishwa na mbegu ya kiume nje ya mwili wa mwanmke. Baada ya hapo Kiumbe kinachofanyika kinapandikizwa kwenye kizazi kiweze kukua.
Uamuzi wa Kupandikiza Mimba Unatofautiana
Teknolojia hii unaweza kuamua kutumia
- yai lako na mbegu ya mme wako
- yai lako na mbegu ya mwanaume mwingine usiyemfahamu ama unayemfahamu
- mayai kutoka kwa mwanamke mwingine na mbegu za mme wako na
- yai na mbegu kutoka kwa watu wengine kisha kiumbe kikapandikizwa kwenye kizazi chako.
- Lakini pia kwa makubaliano maalumu wewe na daktari unaweza kuamua kiumbe kikapandikizwa kwa mwanamke mwingine akalea mpaka kujifungua kisha ukachukua watoto wako bila kubeba mimba.
Chansi ya kufanikiwa kwa IVF ni asilimia 41 mpaka 43 kwa wanawake chini ya umri wa miaka 35. Chansi ya kiumbe kukua na kujifungua salama baada ya upandikizaji inapungua zaidi umri unavoenda.
Kwanini Mimba Zinapandikizwa?
Teknolojia ya IVF ni msaada mkubwa sana kwa wanawake walioshindwa kushika mimba kwa njia ya kawaida. Kupandikiza mimba ni ghali sana, mpaka kufikia hivo maana yake wanandoa wameshajaribu njia nyingi bila mafanikio.
Baadhi ya changamoto za uzazi zinazopelekea wanandoa kuamua kupandikiza mimba ni pamoja na
- kupungua kwa mayai kwa mwanamke wa umri zaidi ya miaka 40
- kuziba kwa mirija ya uzazi
- kupunguza kwa uwezo wa mifuko ya mayai
- vimbe kwenye kizazi (fibroids)
- kutanuka kwa kizazi (endometriosis)
- mwanaume kuwa na mbegu chache na pia
- kushindwa kushika mimba kwa sababu yoyote isiyoogundulika kwa vipimo
Maandilizi Kabla ya Kupandikiza Mimba
Kabla ya kupandikiza mimba mwanamke atafanyiwa vipimo vya mayai. Kipimo hichi hufanyika kwa kuchukuliwa damu na kupima kiwango cha homoni ya follicle stimulating hormone(FSH). Matokeo ya kipimo hiki ndio yatampa daktari mwanga juu ya kiwango na ubora wa mayai yako.
Daktari pia atakupima kizazi chako. Utafanyiwa utrasound kuona kama kizazi kipo vizuri kubeba mimba na pia namna gani daktari apandikize kiumbe kiweze kukua vizuri.
Mwanaume atapimwa mbegu. Daktari atamwelekeza mwanaume kupiga punyeto na kuleta kiwango cha mbegu maabara. Kipimo kitagundua wingi na ubora wa mbegu.
IVF inafanyikaje?
Zifuatazo ni Hatua kuu tano za upandikizaji wa mimba
1.Stimulation
Kikawaida mwanamke anatoa yai moja lililopevuka kwa kila mzunguko wa hedhi. Upandikizaji wa mimba unahitaji mayai mengi yapatikane ili kuongeza chansi ya kutengeneza kiumbe. Daktari atakupatia dawa za kumeza kuchochea uzalishaji wa mayai. Wakati huu daktari ataendelea kukufanyia vipimo mbalimbali vya damu kujua siku gani ya kuchukua yai.
2.Egg Retrieval
Kitaalamu huitwa follicular aspiration. Ni upasuaji mdogo unaofanyika kutoa yai kwenye mfumo wa mayai baada ya kuwekewa nusu kaputi. Daktari atatumia utrasound kuingia sindano kwenye uke, kisha mpaka kwenye mfuko wa mayai. Sindano hii itafyonza mayai na majimaji kwenye mfuko.
3.Insemination
Kwenye hatua hii daktari atachukua mbegu kutoka kwa mwanaume (baada ya kupiga punyeto) kisha mbegu na yai huchanganywa kwenye kifaa maalumu.
4.Embryo Culture
Kiumbe kilichotengenezwa baada ya urutubishaji kitaendelea kupimwa na kufuatiliwa ukuaji wake katika mazingira wezeshi kama yake ya kwenye kizazi.
5.Transfer
Baada ya kiumbe kufikia ukuaji unaotakiwa, ndipo kinaweza kupandikizwa kwa mwanamke. Upandikizi hufanyika kwa kuingiza bomba maamulumu linaloitwa catheter kisha kiumbe kinaingizwa mapaka kwenye kizazi.
Baada ya hapo dakari ataendelea kukufanyia vipimo vya damu baada ya siku 6 mpaka 10 kuona kama mimba tayari imeingia.
Matatizo gani yanaweza Kutokea baada ya Kupandikiza Mimba?
Changamoto za kupandikiza mimba ni pamoja na
- kupata mimba ya watoto mapacha ambayo yaweza kupelekea kujifungua watoto njiti
- mimba kuharibika
- mimba kutunga nje ya kizazi(ectopic)
- kutokwa damu kupita kiasi ama maambukizi ya bakteria kwenye kizazi.