Kupungukiwa damu wakati wa hedhi

Upungufu wa damu unaathiri kiwango cha usafirishaji wa hewa safi ya oksijeni mwilini. Kwenye seli za damu, hewa ya oksijeni hubebwa na kusafirishwa kupitia protini zinazoitwa hemoglobin. Upungufu huu wa damu unasababishwa na vitu vingi, na kimojawapo ni hedhi nzito na ya muda mrefu.

Upungufu wa damu unasababishwa na vitu vikubwa vitatu ambavyo ni

  • kupoteza damu mfano kwenye ajali
  • kupungua uzalishaji wa seli nyekundu za damu na
  • kuharibiwa kwa seli nyekundu za damu

Kupungukiwa madini chuma

Aina mojawapo kuu sana ya upungufu wa damu ni ile inayosababishwa na upungufu wa madini chuma na hivo kupelekea upungufu wa uzalishaji wa damu.

Upungufu wa madini ya chuma inawatokea zaidi wanawake kuliko wanaume. Na vihatarishi vikubwa kwa mwanamke vinavyopelekea upungukiwe madini haya ni pamoja na

  • hedhi nzito na ya muda mrefu
  • ujauzito
  • lishe yenye kiwango kidogo sana cha madini chuma, Vitamin B12 na folate
  • changamoto ya kiafya

Kwenye makala hii tutaelezea kwa kina jinsi gani hedhi nzito inapelekea upungukiwe damu, dalili za kuzifatilia na tiba ya tatizo.

Namna gani hedhi nzito inavyosababisha upungufu wa damu

Pale unapotokwa na damu nyingi sana kwenye hedhi yako, inapelekea kupoteza kiwango kikubwa cha seli nyekundu za damu kuliko kiwango kinachozalishwa na mwili. Hii itapunguza kiwango cha madini chuma. Matokeo yake mwili wako utakuwa kwenye wakati mgumu kusafirisha hewa safi.

Unajuaje kama hedhi yako inaleta upungufu wa damu?

Dalili hizi zinaonesha kwamba hedhi yako ni nzito sana na inachukua muda mrefu kuliko kawaida. Jambo linaloweza kupelekea ukapungukiwa damu

  • unabadilisha zaidi ya pedi moja kwa kila lisaa
  • unahitajika kuvaa pedi mbili ili kunyonza damu
  • unabadilisha pedi nyakati za usiku
  • hedhi ndefu sana zaidi ya siku 7
  • unatokwa na mabonge ya damu kama maini
  • unajiskia uchovu mkubwa sana na
  • kushindwa kabisa kufanya kazi zako nyakati za hedhi
  • Kupata lishe nzuri yenye madini chuma nyakati za hedhi itakusaidia kupunguza hatari ya kupungukiwa damu.

Dalili za kupungukiwa damu

Kama una kiwango kidogo cha hemoglobin kwenye damu, utaanza kupata dalili hizi

  • mwili kuishiwa nguvu mara kwa mara
  • kushindwa kupumua vizuri
  • ngozi kuwa na rangi ya njano
  • kizunguzungu na
  • maumivu ya kichwa

Nini kinasababisha hedhi nzito na ya muda mrefu?

Hedhi nzito inaweza kusababishwa na kuvurugika kwa homoni, hasa homoni za progesterone na estrogen. Sababu zingine ni pamoja na

  1. Vimbe kwenye kizazi-fibroids
  2. Kizazi kupanuka
  3. Changamoto kwenye upevukaji wa mayai
  4. Matumizi ya kitanzi kupanga uzazi
  5. Baadhi ya dawa mfano asprin

Lini unatakiwa kumwona Daktari

Hakikisha unaenda hospitali haraka endapo

  • unahisi kuchoka kila mara, kizunguzungu na kukosa pumzi wakati wa baada ya hedhi
  • unaaacha kazi zako kutokana na hedhi
  • hedhi inatoka siku nyingi zaidi ya siku saba
  • unatokwa na mabonge ya damu iliyoganda
  • unatumia zaidi ya pedi moja kwa kila lisaa au masaa mawili

Tiba ya upungufu wa damu kutokana na hedhi

Matibabu kwa changamoto yako yatategemea na chanzo cha kutokwa na damu nyingi. Daktari anaweza kukupa dawa za uzazi wa mpango kurekebisha homoni au virutubish vyenye madini chuma na pia kukushauri ule zaidi vyakula vyene madini chuma.

Changamoto inapokuwa kubwa zaidi, itahitaji ufanyiwe upasuaji hasa kama una uvimbe kwenye kizazi. Mara chace zaidi yaweza kupendekezwa utolewe kizazi kabisa.

Hatua za kufuata ili kuzuia upungufu wa damu nyakati za hedhi

Njia nzuri ya kupunguza hatari ya kuishiwa damu ni kuzingatia swala la lishe. Jaribu njia hizi

  1. Kula zaidi vyakula vyenye madini chuma kwa wingi. Vyakula hivi ni pamoja na nyama, maini, spinach, samaki na maziwa
  2. Kula zaidi vyakula vinavyoongeza uwezo wa mwili kufyonza madini chuma. Vitami C kutokwa kwenye vyakula kama machungwa, broccoli, limau na mapera.
  3. Punguza vyakula vinavyozuia ufyonzaji wa madini chuma. Vyakula vye caffeine kama kahawa na chai ra rangi na vonywaji vyenye sukari nyingi kama soda

Kama unatumia virutubishi vya calcium hakikisha unapata na virutubishi vya madini chuma, kwani calcium hupunguza ufyonzaji wa madini chuma.

Vitu gani vingine vinapunguza damu?

Kuna sababu zingine nyingi zinazoweza kupelekea mtu apungukiwe damu. Baadhi ni pamoja na

  • Matumizi madogo ya vyakula vyenye madini chuma
  • Majeraha ndani ya mwili
  • Ujauzito
  • Kiwango kidogo cha Vitamin B12
  • Magonjwa ya mifupa-bone marrrow disease kama saratani ya damu
  • Kurithi vinasaba mfano sickle cell– ambapo mwili unazalisha seli za damu zisizo na hemoglobin.
  • Magonjwa sugu kama ukimwi, na magonjwa ya figo.

Hitimisho

Hedhi nzito na ya muda mrefu inaweza kuathiri kiwango chako cha damu. Kwa wanawake wengi changamoto hii inaweza kutibiwa na kuisha mapema. Kama una dalili za kupungukiwa damu hakikisha unaenda hospitali na kumwona daktari. Daktari atakufanyia tathmini na vipimo kujua chanzo cha tatizo lako kabla hajaamua kukuanzishia dawa.