Magonjwa ya zinaa ama sexually transmitted disease(STD) yanajumuisha magonjwa yote yanayosambazwa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kupitia ngono. Magonjwa haya haimaanishi kwamba huwezi kuyapata kwa njia zingine, ila tu njia ya ngono ni njia kubwa zaidi.
Dalili za Magonjwa ya zinaa kwa mwanaume
Inawezekana kabisa kuugua ugonjwa wa zinaa pasipo mwili kuonyesha dalili. Lakini magonjwa mengi huleta dalili hizi kwa wanaume
- Maumivu wakati wa kukojoa na tendo la ndoa
- Malengelege na vidonda sehemu za siri
- Kutokwa na uchafu usio wa kawaida kwenye uume
- Kuvimba kwa mapumbu ikiambatana na maumivu makali
Dalili za magonjwa ya zinaa kwa Mwanamke
Kwa kiasi kikubwa dalili huchelewa kujionesha kwa wanawake baada ya kupata maambukizi. Endapo dalili zitajitokeza zitakuwa kama
- Maumivu wakati wa tendo na kukojoa
- Muwasho ukeni
- Kutokwa uchafu usio kawaida ukeni
- Malengelenge na vipele sehemu za siri na mdomoni
Aina za magonjwa ya zinaa
Kuna aina nyingi za magonjwa ya zinaa ambayo huambukizwa kwa kufanya ngono. Tutazungumzia aina kuu nne ambazo watu wanaugua zaidi.
1.Kaswende (Syphilis)
Kaswende ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria. Maambukizi ya ugonjwa hayaonekani kwa hatua za mwanzo mpaka pale unaposambaa zaidi. Dalili kubwa ya kwanza ambayo utaiona baada ya kuugua kaswende ni kupata lengelenge lisilouma la duara kwenye sehemu za siri, mkundu ama mdomoni.
Dalili zingine za kaswende zitakazofuata ni pamoja na
- Mwili kukosa nguvu
- Homa kali
- Maumivu ya kichwa
- Maumivu ya joints
- Kupungua uzito ghafla na
- Nywele kunyonyoka
Kama kaswende isipotibiwa mapema inaweza kupelekea
- Kupofuka macho
- Kupoteza kumbukumbu
- Magonjwa ya moyo
- Kupoteza uwezo wa kusikia na
- Maambukizi kwenye ubongo
Kwa bahati nzuri ni kwamba kaswende ikigundulika mapema inatibika kupitia antibiotics. Japo kwa wanawake wenye ujauzito kaswende ni hatari zaidi, ndiomaana ni muhimu sana mjamzito kupimwa kama ana kaswende.
2.Ukimwi
Ukimwi unaathiri kinga yako na hivo kukufanya kuwa dhaifu kwa magonjwa mengine nyemelezi kama saratani na TB. Lakini kutokana na kukua kwa teknolojia ya tiba, hivi sasa kuna dawa za kupunguza makali ya virusi na mgonjwa akaishi miaka mingi zaidi.
Katika hatua za awali ni rahisi sana kuchanganya dalili za mafua makali na dalili za ukimwi. Mfano wa dalili za mwanzo kabisa za ukwimwi ambazo hufanana na dalili za mafua makali ni pamoja na
- homa kali
- maumivu ya joints
- kuvimba mtoki
- maumivu ya kichwa
- kichefuchefu na
- Koo kukauka na kuwasha
Dalili hizi zinaweza kupotea baada ya miezi kadhaa. Na baada ya hapo inaweza kuchukua miaka ndipo uanze kuugua. Mpaka sasa bado hakuna tiba ya ukimwi, ila kuna dawa za kupunguza makali ya virusi. Mgonjwa akizingatia tiba vizuri ataishi miaka mingi.
Pia mgonjwa akitumia dawa vizuri inapunguza uwezekano wa kumwambukiza mwingine.
Upimaji wa ukimwi unafanyika hospitali zote. Kama una hofu kwamba waweza kuwa umepata maambukizi, usihofu kwenda hospitali kupima kupata uhakika wa afya yako.
3.Kisonono ama Gonorrhea
Watu wengi hupata kisonono na kutoonesha dalili mwanzoni. Kama dalili zitakuja zitaambatana na
- Kutokwa na uchafu wa njano ama kijani kwenye uke ama uume
- Maumivu makali wakati wa kukojoa na wakati wa tendo
- Kukojoa mara kwa mara
- Muwasho sehemu za siri
- Kukauka koo na kuwasha
Endapo kisonono hakitatibiwa mapema inaweza kupelekea maambukizi kwenye njia ya mkojo, kordani na tezi dume PID na Ugumba
Inawezekana kwa mama mjamzito kumwambukiza mtoto wakati wa kujifungua. Endapo itatokea hivo, kisonono kinaweza kuleta matatizo makubwa zaidi kwa mtoto. Ndiomaana wajawazito wanashauriwa kufanya vipimo mara kwa mara kuhusu magonjwa ya zinaa.
Habari njema ni kwamba kisonono kinatibika kupitia antibiotics.
4.Trichomoniasis
Trichomoniasis husababishwa na vimelea wadogo wanaoambukizwa kupitia ngono. Dalili zake ni pamoja na
- Kutokwa na uchafu kwenye uke au uume
- Muwasho na kuwaka moto kwenye uke au uume
- Kokojoa mara kwa mara na
- Maumivu wakati wa tendo na mkojo
Kwa wanawake uchafu unaotoka ukeni huwa na harufu kali kama shombo la samaki. Endapo ugonjwa hautatibiwa mapema unaweza kusababisha
- Maambukizi kwenye njia ya mkojo
- PID na
- Ugumba
Trichomoniasis pia inaweza kutibiwa mapema kwa antibiotics kama utawahi hospitali