Tatizo la Preeclampsia ni pale mjamzito anapokuwa na presha kubwa ya damu, kiwango kikubwa cha protini kwenye mkojo na kuvimba miguu na mikono. Inaweza kutokea kikawaida ama hali ikawa mbaya zaidi na kupelekea kifafa cha mimba. Hali hii ya mjamzito kuvimba miguu hujitokeza ujauzito unapokuwa mkubwa wa wiki sita.
Japo kwa wanawake wachache yaweza kujitokeza mimba ikiwa changa ama baada tu ya kujifungua.
Kifafa Cha Mimba
Kuongezeka huku kwa shinikizo la damu kunaweza kupelekea kifafa cha mimba, tatizo ambalo ni hatari zaidi linaweza kusababisha kifo cha mama na mtoto. Tiba pekee ya preeclampsia ni pale mwanamke anapojifungua. Ukishajifungua shinikizo la damu litapungua na miguu na mikono itaacha kuvimba ndani ya week 6 za mwanzo.
Kujilinda na madhara ya kuongezeka huku kwa shinikizo la damu na kuvimba viungo kwa mjamzito muhimu ufahamu dalili zake, lakini pia kutembelea kliniki mara kwa mara.
Dalili Na Viashiria Vya Mjamzito Kuvimba Miguu
Ukiacha dalili za kuvimba miguu na mikono, kuongezeka presha ya damu, dalili zingine za preeclampsia ni pamoja na
- kuongezeka uzito kutokana na kuongezeka kwa maji mwilini
- maumivu ya tumbo hasa eneo la juu kulia
- maumivu makali ya kichwa
- kupata mkojo kidogo
- uchovu kupita kiasi
- kutapika na kichefuchefu kupitiliza
- uwezo wa kuona kupungua yaani kuona maruerue.
Baadhi ya wanawake wenye preeclampsia hawapati dalili zozote, kwahivo ni muhimu sasa kumwona daktari mara kwa mara ili kupata vipimo vya damu na mkojo.
Lini Dalili Za Mjamzito Kuvimba Miguu huanza Kuonekana?
Dalili za kuvimba miguu na mikono kwa baadhi ya wajawazito huanza kuoneakana ndani ya week 20 za mwanzo, lakini wengi wao huanza kuona baada ya week 34(miezi nane). Wanawake wachache zaidi wanaweza kupata dalili za preeclampsia baada hata ya kujifungua ndani ya masaa 48 baada ya kujifungua. Ukiona dalili hizi baada ya kuzaa wala usiwe na hofu zitaisha ndani ya week 12.
Nini Kinasababisha Kuvimba Miguu, Mikono na Kuongezeka Presha Kwa Mjamzito?
Wataalamu wa magonjwa ya wanawake wanafikiri tatizo hili pamoja na kifafa cha mimba husababishwa na kutofanya kazi vizuri kwa kondo la nyuma(placenta). Baadhi ya wataalamu wanafikiri lishe mbovu na mafuta mengi mwilini vinaweza kuwa sababu. Kupungua kwa usafirishaji wa damu kuelekea kwenye kizazi ni sababu pia.
Mazingira hatarishi Yanayosababisha Upate Preeclampsia ni pamoja na
- kubeba mimba katika umri zaidi ya miaka 40
- wajawazito kwa mara ya kwanza
- kushika mimba zaidi ya moja ndani ya miaka miwili au zaidi ya miaka 10
- kuugua presha kabla ya kushika ujauzito
- kuwahi kuugua preeclampsia hapo mwanzo
- historia ya wanafamilia kuugua preeclampsia mfano mama au dada
- historia ya kuwa na uzito mkubwa na kitambi
- kubeba mimba ya mapacha
- kupata mimba kwa kupandikiza(in-vitro fertilization)
- Historia ya kuugua magonjwa ya kisukari, figo na baridi yabisi
Madhara Makubwa Ya Mjamzito Kuvimba Miguu na Presha Kupanda
Kuongezeka kwa presha ya damu na hivo kuvimba miguu na mikono kwa mjamzito kunaweza kupelekea kupungua kwa damu kwenye kondo la nyuma na hivo mtoto kuzaliwa na uzito mdogo sana. Kitaalamu inaitwa fetal growth restriction.
Ni chanzo kimojawapo cha mama kujifungua kabla ya muda wake na hivo kupelekea madhara mengine kwa mtoto, kama uwezo mdogo wa ubongo, kifafa, uwezo mdogo wa kuona na kusikia.
Madhara ya Preeclampsia kwa mama
Kwa mjamzito au mama aliyejifungua preeclampsia inaweza kupelekea matatizo kama
- kiharusi
- kifafa
- kujikusaya kwa maji kwenye kifua
- moyo kushindwa kufanya kazi
- kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua
Preeclampsia pia yaweza kusababisha kondo la nyuma kukatika na hivo mtoto kukosa kabisa lishe na hewa na hivo kuzaa njiti.
Tiba Kwa Tatizo la Preeclampsia
Tiba pekee ya kuvimba miguu na mikono ukiwa na mimba pamoja na kifafa cha mimba ni kujifungua. Daktari katika kufatilia afya ya mtoto tumboni atakupa maelekezo siku gani yatakiwa ujifungue kwa kulingana na ukubwa wa tatizo lako.
Kama mtoto ana afya nzuri, katimiza week 37 au zaidi daktari anaweza kukupa sindano ya uchungu ili uzae mapema ama akapendekeza akufanyie upasuaji. Itakusaidia usipate kifafa cha mimba na kupoteza watoto bure.
Uzito Salama wa Mtoto
Kama mtoto hajakamilika, daktari ataendelea kukupa dawa kutibu dalili za preeclampsia mpaka pale mtoto atakapofikia afya njema kuzaliwa. Kumbuka unapozaa mtoto katika wiki zaidi ya 37 ndipo unaongeza chansi ya mtoto kuwa na afya njema zaidi.
Kama una dalili ndogo ndogo zisizo serious sana daktari anaweza kupendekeza bed rest, aidha hospitali ama nyumbani kwako (muda mwingi upumzike ukiwa umelalia upande wa kushoto. Wakati huo daktari anaendelea kuchukua vipimo vyako vya damu, mkojo na presha ya damu na kukupa dawa kupunguza presha.
Nini ufanye kama kinga kwa tatizo la mjamzito kuvimba miguu
Kama upo kwenye makundi ya wenye hatari zaidi ya kupata preeclampsia unapaswa kufanya haya
- kupunguza uzito kama una uzito mkubwa
- kuacha kuvuta sigara
- kufanya mazoezi mara kwa mara
- fanya vipimo mara kwa mara kuhakikisha presha na sukari yako iko normal
Hakikisha tu usitumie dawa na virutubisho vyovyote bila kuongea na daktari wako.