Umewahi kuugua mafua ya muda mrefu bila kuisha? au kuziba kwa pua kila mara pasipo kupona. Pamoja na kumeza dawa za famasi za aleji lakini tatizo haliishi? Pengine una tatizo la kuota nyama za pua na hujui.
Nyama za pua ni vimbe zisizo saratani (benign) ambazo zinaota kwenye tishu laini za ndani ya pua yako.
Nini kinasababisha kuota nyama za pua?
Nyama za pua zinaota kwenye ukuta laini wa ndani ya pua, ukuta huu unaitwa mucosa. Mucosa ni ukuta laini na wenye majimaji muda wowote. Kazi yake ni kulinda pua na pia kuweka unyevunyevu kwenye hewa unayoivuta.
Endapo pua imepatwa na maambukizi ama una aleji yoyote, ukuta wa mucosa unavimba na kuwa mwekundu. Na unaweza kuzalisha majimaji yanayotoka nje. Kadiri ukuta huu unavotutumka zaidi unaweza kutengeneza vinyama (polyp). Polyp ni kinyama cha duara kinachoziba njia za hewa na kukufanya ushindwe kupumua vizuri.
Mazingira hatarishi yanayopelekea kuota nyama za pua
Japo baadhi ya watu wanaweza kupata nyama za pua hata kama hawakuwahi kuugua magonjwa ya pua, kuna vihatarishi vinavyopeleka tatizo. Vihatarishi hivi ni pamoja na
- kuumwa pumu
- aleji
- maambukizi kwenye njia ya hewa mara kwa mara na
- mwili kukataa baadhi ya dawa kama ibuprofen na asprin
Dalili gani zinaonesha una nyama za pua?
Nyama za pua ni vimbe laini zisizoleta maumivu ndani ya njia za pua. Nyama hizi hukua hasa ndani ya pua ambapo mfupa wa macho na pua vinapokutana. Wakati mwingine ni ngumu kabisa kujua kama una nyama za pua kwasbaabu hazina neva za kusafirisha taarifa kwenda kwenye ubongo.
Nyama hizi za pua zinaweza kukua kupita kiasi hadi kuziba pua na kusababisha ushindwe kutoa makamasi vizuri. Dalili zake ni pamoja na
- kuhisi kama pua zako zimeziba na kushindwa kuvuta hewa
- mafua yasiyoisha
- pua kukauka
- kupungua kwa uwezo wa kunusa
- kuvuta hewa kupitia mdomo
- kuhisi kama mgandamizo kwenye paji la uso
- kukosa usingizi mtamu
- kukoroma usingizini
Maumivu pia ya kichwa yanaweza kujitokeza endapo una mamabukizi kwenye njia ya pua.
Vipimo kugundua nyama za pua
Daktari atatumia kifaa kinachoitwa nasoscope kutazama ndani ya pua zako kama kuna uvimbe. Kama uvimbe ni mrefu kuendekea ndani zaidi ya pua, daktari atatumia endoscopy, kifaa cha kuingiza ndani ya pua.
Daktari anaweza pia kupendekeza ufanyiwe CT scan au MRI kujua hasa ukubwa wa nyama za pua. Pia vipimo hivi vitaonyesha kama vimbe zimefanya kupinda kwa mifupa laini ya kwenye pua.
Daktari pia anaweza kupendekeza kipimo cha aleji kujua chanzo cha kututumka kwa pua zako mara kwa mara.
Tiba kwa ajili ya tatizo la kuota nyama za pua
Tiba ya kwanza ni dawa: Dawa zitasaidia kupunguza ukubwa wa nyama za pua na pia kuzibua njia za pua uweze kuvuta hewa vizuri.
Dawa za steroid za kumeza ama sindano mfano prednisone, zinaweza kusaidia kupunguza hali ya kuvimba kwa pua.
Anthistamine zinaweza kutumika kama una aleji, pia antibiotics kama una maambukizi ya bakteria.
Upasuaji: Kama dalili zako bado haziishi hata baada kutumia dawa, kuna haja ya kufanyiwa upasuaji. Aina ya upasuaji itategemeana na ukubwa wa nyama zako za pua.
Ni yapi madhara makubwa ya nyama za pua?
Kutibu nyama za pua hasa kwa upasuaji inaweza kupelekea kuvuja damu sana. Upasuaji pia unaweza kupelekea upate maambukizi. Hakikisha unaendelea kutumia dawa ulizopatiwa hospitali ili kupunguza hatari ya kupata maambukizi.