Mwili wako unapitia mabadiliko makubwa sana wakati wa ujauzito. Hata baada ya kuzaa kuna mabadiliko utaendelea kuyaona kwenye afya yako ya uzazi. Moja ya mabadiliko unayoweza kuyapata ni uke mkavu baada ya kujifungua.
Wanawake wengi hupatwa na tatizo hili na hivo kuwafanya washindwe kufurahia tendo la ndoa kwani wanapata maumivu makali.
Mabadiliko ya homoni na Uke Mkavu baada ya Kujifungua
Mabadiliko ya Homoni yanavyochangia uke kuwa mkavu.
Homoni hizi za estrogen na progesterone zinamchango mkubwa katika tatizo lako la kuwa mkavu.
Homoni hizi ndizo zinaamrisha mwili kufanya kazi mbambali za uzazi kama lini upate balehe, kukua kwa matiti, hamu ya tendo la ndoa, ukuaji wa uke, hedhi yako, mayai kupevuka na hata uzalishaji wa uteute ukeni.
Kiwango cha homoni hizi hupungua sana masaa 24 baada ya kuzaa na kurudi katika hali ya mwanzo ulivyokuwa kabla ya kushika mimba. Utakapoanza kunyonyesha pia homoni ya estrogen itapungua zaidi maana inaathiri uzalishaji wa maziwa endapo itakuwa nyingi.
Umuhimu wa Estrogen Kwenye Hamu ya Tendo
Fahamu tu kwamba homoni ya estrogen ni muhimu katika kukupa msisimko wa tendo la ndoa. Kwani inaimarisha mzunguko wa damu kuelekea kwenye via vya uzazi na pia kulainisha uke wako. Kupungua kwa homoni ya estrogen ndio chanzo kikubwa cha uke wako kuwa mkavu baada ya kujifungua.
Baadhi ya wanawake huanza kutumia virutubishi vyenye estrogen. Wengine huamua kutotumia kabisa kwani virutubishi hivi vinaongeza hatari ya kuugua saratani. Zungumza na daktari akupe ushauri kwanza kabla hujaamua kutumia virutubishi hivi.
Matatizo ya Tezi Ya Thyroid(postpartum thyroiditis)
Uke mkavu baada ya kujifungua inaweza kusababishwa na matatizo ya tezi ya shingoni inaitwa thyroid. Tezi hii ya shingoni inazalisha homoni ama vichocheo vinavyoamrisha shuguli mbalimbali za mwili.
Inapotokea tezi ya thyroid kuzalisha homoni nyingi kupita kiasi ama kidogo kupita kiasi ndipo shida inapoanza. Dalili za shida kwenye thyroid ni pamoja na
- mwili kutetemeka
- kushindwa kupata usingizi mzuri
- kuongezeka uzito sana
- mwili kukosa nguvu
- ngozi kukauka
- uke kuwa mkavu sana
- kuhisi baridi hata wakati wa joto
Wanawake wengi wanaugua Tezi ya Shingoni
Endapo unapata dalili hizi na zingine jua kwamba haupo peke yako na usife moyo. Asilimia kumi ya wanawake wanaojifungua wanapata tatizo hili. Aina ya tatizo ulilonalo ndilo litamfanya daktari achague tiba gani ni sahihi zaidi kwako.
Kwa wanawake wengi wanapona tatizo wakishaanzishiwa dawa ndani ya miezi 12 mpaka 18. Hakikisha unaenda hospitali haraka endapo utaona dalili hizi.
Nini cha kufanya ukiwa na uke mkavu
Fahamu kwamba bado una uwezo wa kufurahia tendo la ndoa hata kama una uke mkavu. Dondoo hizi hapa chini zitakusaidia kupunguza makali ya tatizo wakati unajiandaa kumwona daktari.
- Tumia vilainishi kama KY gel wakati wa tendo la ndoa.
- Ongea na dakari kuhusu kutumua estrogen vaginal cream.
- Kunywa maji ya kutosha kila siku.
- Usitumie sabuni wa marashi ukeni.
- Ongea na mwenzi wako kuhusu tatizo ili akuvumilie wakati unatafuta tiba.
- Jaribu staili mbalimbali ya tendo upate inayokufaa, hakikisha pia unatumia muda mrefu wa kuaandanaa kabla ya kuingiliwa na mwanaume.
Lini unatakiwa Kumwona daktari
Siku zote ongea na mtaalamu wa magonjwa wa wanawake unapooona mwili wako haupo sawa hasa kwenye via vya uzazi. Endapo utaona uke unazidi kuwa mkavu zaidi pamoja na kuzingatia ushauri hapo juu usikae kimya, muone daktari mapema.
Maambukizi ya bakteria na fangas, na magonjwa kama kisukari yanaweza kusababisha uke kuwa mkavu. Kwahivo ni muhimu kupata ushauri wa daktari na kuwa mkweli unapozungumza na mtoa huduma apate kukusaidia.
Kwa vyovyote vile unavojiikia kwa ukavu wako ukeni usijutie, jua tu kwamba haupo peke yako na utapona.