Covid-19 ni ugonjwa wa mfumo wa hewa unaosababishwa na virusi vya corona. Baadhi ya watu wanaweza kupata maambukizi ya virusi na wasione dalili zozote hatua hii huitwa asymptomatic. Watu wengi hupata dalili za kati na hupona bila hata ya kupata tiba. Ila watu wachache hupata dalili mbaya sana kama kushindwa kupumua na wanahitaji usimamizi mkubwa wa madaktari hospitali.
Endapo una magonjwa mengine kama kisukari, pumu , ukimwi na magonjwa ya moyo, upo kwenye hatari zaidi ya kupata dalili mbaya, utakapougua corona.
Dalili kuu za ugonjwa wa virusi vya corona
Dalili kubwa zinazowatokea watu wengi wanaopata maambukizi ya corona ni kama
- homa kali
- kikohozi kikavu na kukosa pumzi
- kuhisi uchovu sana
- maumivu ya kichwa
- kukosa uwezo wa kunusa na ladha
- koo kukauka
- pua kuwasha na kuziba
- kichefuchefu na kutapika na
- kuharisha
Kumbuka dalili hizi zinaweza kukuanza siku ya pili mpaka siku ya 14 baada ya kuambukizwa.
Dalili mbaya zinazohitaji upelekwe hospitali haraka
Endapo una dalili hizi, nenda hospitali haraka upate usaidizi wa daktari
- kushindwa kupumua vizuri
- maumivu makali ya kifua mara kwa mara
- lips na uso kuwa kama blue
- kushindwa kutamka maneno vizuri
Pia imeripotiwa kwa baadhi ya wagonjwa kupata stroke baada ya kuugua ugonjwa wa corona. Kujua kama mgonjwa amepata stroke tazama maeneo haya
- Uso: tazama kama upande mmoja wa uso umeshuka chini
- Mkono: je mkono mmoja haufanyi kazi? tazama kama mgonjwa anaweza kunyanyua na kushusha mkono
- Kuongea: Je mgonjwa anaongeza vizuri? mwambie atamke neno kwa kulirudia
Kumbuka kwamba kupona kwa mgonjwa wa stroke, kunategemea ni kwa kiasi gani amewahishwa hospitali. Kuchelewa kuanza tiba kunapunguza chansi ya kupona.
Dalili zingine za ugonjwa wa corona
Covid-19 inaweza kuleta matatizo mengine kama
- macho kuwa na wekundu na kuvimba
- kupoteza fahamu
- kukohoa damu
- damu kuganda
- matatizo ya moyo
- changamoto za figo na
- kuathirika kwa ini
Nini cha kufanya endapo umegundua kwamba una dalili za corona
Kama una dalili za mwanzo za corona kama homa, kukosa pumzi au kukohoa, fanya mambo haya.
- Tulia nyumbani muda wote, labda tu ukiwa unaenda hospitali ndipo utoke.
- Mjulishe daktari kuhusu maendeleo ya ugonjwa wako, na pia kama upo kwenye makundi hatarishi
- Jitenge na watu wengine: hata ndugu zako wa nyumbani unatakiwa kukaa nao mbali ili usiwaambukize. Tumia chumba cha peke yako na choo chako.
- Vaa barakoa ama kitambaa cha kuziba mdomo na pua endapo itakulazimu kutembetembea na kuongea na watu.
- Pumzika na unywe maji ya kutosha, unaweza pia kumeza dawa za maumivu na kikohozi kutuliza hali yako
- Fuatilia kwa makini dalili zako, kama zitakuwa mbaya unahitaji kupata msaada wa daktari.
Lini ni muda sahihi wa kwenda kupima corona?
Kama bado hujapata chanjo ya corona, unahitaji kufanyiwa vipimo endapo
- umeanza kuona dalili za corona
- uliambatana na mgonjwa wa corona na kusogeleana nae kwa zaidi ya dakika 15
- ulikuwa kwenye mkusanyiko mkubwa
- eneo lako la kazi linakuhitaji kufanyiwa kipimo
Kama tayari umepata chanjo na unahisi kama una dalili za corona, mpigie daktari ama enda hospitali haraka kupata mwongozo.
Kuna tofauti gani kati ya dalili za covid-19, mafua na aleji?
Pamoja na kwamba changamoto hizi zinaendana kwa dalili nyingi, inaweza kuwa ngumu kutofautisha dalili na kujua nini hasa kinakusumbua. mwongozo huu hapa chini kwenye jedwali utakusaidia kutofautisha.
Dalili | Mafua | Aleji | Covid-19 |
homa | kali(siku 3mpaka 4) | hakuna | kawaida |
maumivu ya kichwa | makali | hakuna | kawaida |
maumivu ya mwili kiujumla | kawaida | hakuna | kawaida |
kukosa nguvu | hali mbaya(wiki 2-3) | mara chache | kidogo |
mafua makali ya maji | kawaida | hakuna | inaweza kutokea |
kupiga chafya | mara chache | kawaida | haijaripotiwa |
koo kukauka | inatokea | mara chache | haijaripotiwa |
kukohoa | kawaida | mara chache | inatokea |
kukosa pumzi | mara chache sana | inatokea kwa pumu | inatokea sana |
Jinsi ya kujilinda mwenyewe
Endapo bado hujapata chanjo, hakikisha unachukua tahadhari zifuatazo
- Osha mikono kwa maji tiririka na sabubi kwa sekunde 30 kila muda
- Tumia sanitizer zilizoidhinishwa na shirika la dawa na chakula TMDA
- Vaa barakoa muda wote unapokuwa kwenye misongamano
- Kaa mbali na watu wenye dalili za corona
- Usishike pua, wala mdomo wako kama hujanawa au kupakaa sanitizer
Kama unamuhudumia mgonjwa wa corona, hakikisha unachukua tahadhari zifuatazo.
- vaa barakoa muda wote mnapoongea na mgonjwa
- hakikisha mgonjwa wako anavaa barakoa muda wote unapomuhudumia
- usikae chumba kimoja na mgonjwa, muhudumie kisha muache kwenye chumba chake
- vaa gloves muda wote unapomuhudumia mgonjwa chakula
- usichangie vifaa kama simu, chakula na hata kitanda
- kila mara safisha eneo anaolala mgonjwa na kupuliza dawa.
- kula vizuri na upate kupima mara kwa mara kama una corona.