Dalili za Corona, Covid-19 na ushauri wa kufuata

dalili za corona
virusi vya corona

Covid-19 ni ugonjwa wa mfumo wa hewa unaosababishwa na virusi vya corona. Baadhi ya watu wanaweza kupata maambukizi ya virusi na wasione dalili zozote hatua hii huitwa asymptomatic. Watu wengi hupata dalili za kati na hupona bila hata ya kupata tiba. Ila watu wachache hupata dalili mbaya sana kama kushindwa kupumua na wanahitaji usimamizi mkubwa wa madaktari hospitali.

Endapo una magonjwa mengine kama kisukari, pumu , ukimwi na magonjwa ya moyo, upo kwenye hatari zaidi ya kupata dalili mbaya, utakapougua corona.

Dalili kuu za ugonjwa wa virusi vya corona

Dalili kubwa zinazowatokea watu wengi wanaopata maambukizi ya corona ni kama

  • homa kali
  • kikohozi kikavu na kukosa pumzi
  • kuhisi uchovu sana
  • maumivu ya kichwa
  • kukosa uwezo wa kunusa na ladha
  • koo kukauka
  • pua kuwasha na kuziba
  • kichefuchefu na kutapika na
  • kuharisha

Kumbuka dalili hizi zinaweza kukuanza siku ya pili mpaka siku ya 14 baada ya kuambukizwa.

Dalili mbaya zinazohitaji upelekwe hospitali haraka

Endapo una dalili hizi, nenda hospitali haraka upate usaidizi wa daktari

  • kushindwa kupumua vizuri
  • maumivu makali ya kifua mara kwa mara
  • lips na uso kuwa kama blue
  • kushindwa kutamka maneno vizuri

Pia imeripotiwa kwa baadhi ya wagonjwa kupata stroke baada ya kuugua ugonjwa wa corona. Kujua kama mgonjwa amepata stroke tazama maeneo haya

  • Uso: tazama kama upande mmoja wa uso umeshuka chini
  • Mkono: je mkono mmoja haufanyi kazi? tazama kama mgonjwa anaweza kunyanyua na kushusha mkono
  • Kuongea: Je mgonjwa anaongeza vizuri? mwambie atamke neno kwa kulirudia

Kumbuka kwamba kupona kwa mgonjwa wa stroke, kunategemea ni kwa kiasi gani amewahishwa hospitali. Kuchelewa kuanza tiba kunapunguza chansi ya kupona.

Dalili zingine za ugonjwa wa corona

Covid-19 inaweza kuleta matatizo mengine kama

  • macho kuwa na wekundu na kuvimba
  • kupoteza fahamu
  • kukohoa damu
  • damu kuganda
  • matatizo ya moyo
  • changamoto za figo na
  • kuathirika kwa ini

Nini cha kufanya endapo umegundua kwamba una dalili za corona

Kama una dalili za mwanzo za corona kama homa, kukosa pumzi au kukohoa, fanya mambo haya.

  1. Tulia nyumbani muda wote, labda tu ukiwa unaenda hospitali ndipo utoke.
  2. Mjulishe daktari kuhusu maendeleo ya ugonjwa wako, na pia kama upo kwenye makundi hatarishi
  3. Jitenge na watu wengine: hata ndugu zako wa nyumbani unatakiwa kukaa nao mbali ili usiwaambukize. Tumia chumba cha peke yako na choo chako.
  4. Vaa barakoa ama kitambaa cha kuziba mdomo na pua endapo itakulazimu kutembetembea na kuongea na watu.
  5. Pumzika na unywe maji ya kutosha, unaweza pia kumeza dawa za maumivu na kikohozi kutuliza hali yako
  6. Fuatilia kwa makini dalili zako, kama zitakuwa mbaya unahitaji kupata msaada wa daktari.

Lini ni muda sahihi wa kwenda kupima corona?

Kama bado hujapata chanjo ya corona, unahitaji kufanyiwa vipimo endapo

  • umeanza kuona dalili za corona
  • uliambatana na mgonjwa wa corona na kusogeleana nae kwa zaidi ya dakika 15
  • ulikuwa kwenye mkusanyiko mkubwa
  • eneo lako la kazi linakuhitaji kufanyiwa kipimo

Kama tayari umepata chanjo na unahisi kama una dalili za corona, mpigie daktari ama enda hospitali haraka kupata mwongozo.

Kuna tofauti gani kati ya dalili za covid-19, mafua na aleji?

Pamoja na kwamba changamoto hizi zinaendana kwa dalili nyingi, inaweza kuwa ngumu kutofautisha dalili na kujua nini hasa kinakusumbua. mwongozo huu hapa chini kwenye jedwali utakusaidia kutofautisha.

DaliliMafuaAlejiCovid-19
homakali(siku 3mpaka 4)hakunakawaida
maumivu ya kichwamakalihakunakawaida
maumivu ya mwili kiujumlakawaidahakunakawaida
kukosa nguvuhali mbaya(wiki 2-3)mara chachekidogo
mafua makali ya majikawaidahakunainaweza kutokea
kupiga chafyamara chachekawaidahaijaripotiwa
koo kukaukainatokeamara chachehaijaripotiwa
kukohoakawaidamara chacheinatokea
kukosa pumzimara chache sana inatokea kwa pumu inatokea sana
jedwali kutofautisha dalili za aleji, mafua na virusi vya corona

Jinsi ya kujilinda mwenyewe

Endapo bado hujapata chanjo, hakikisha unachukua tahadhari zifuatazo

  • Osha mikono kwa maji tiririka na sabubi kwa sekunde 30 kila muda
  • Tumia sanitizer zilizoidhinishwa na shirika la dawa na chakula TMDA
  • Vaa barakoa muda wote unapokuwa kwenye misongamano
  • Kaa mbali na watu wenye dalili za corona
  • Usishike pua, wala mdomo wako kama hujanawa au kupakaa sanitizer

Kama unamuhudumia mgonjwa wa corona, hakikisha unachukua tahadhari zifuatazo.

  • vaa barakoa muda wote mnapoongea na mgonjwa
  • hakikisha mgonjwa wako anavaa barakoa muda wote unapomuhudumia
  • usikae chumba kimoja na mgonjwa, muhudumie kisha muache kwenye chumba chake
  • vaa gloves muda wote unapomuhudumia mgonjwa chakula
  • usichangie vifaa kama simu, chakula na hata kitanda
  • kila mara safisha eneo anaolala mgonjwa na kupuliza dawa.
  • kula vizuri na upate kupima mara kwa mara kama una corona.

Soma zaidi -Je kukosa uwezo wa kunusa na kutambua ladha ni dalili ya corona?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *