Ngiri ni kitu gani?
Ngiri au hernia inatokea baada ya kiungo kimoja cha mwili kinapoota na kusukuma eneo dhaifu la ngozi inayoshikilia kiungo hicho.
Aina nyingi za ngiri hutokea eneo la tumbo kati ya kifua na nyonga. Kwa watu wengi ngiri siyo tatizo linalohatarisha maisha japo ni tatizo lisiloisha lenyewe bila upasuaji.
Dalili za Ngiri(hernia)
Dalili kubwa za ngiri ni uvimbe kwenye eneo husika. Mfano kwa mshipa wa ngiri utaona uvimbe pembeni ya kinena kulia au kushoto ama kote. Utaweza kujihisi kama una ngiri endapo utakohoa, kucheka, na unaposimama kwasababu huleta maumivu makali sana.
Aina zingine za hernia kama hital ambayo hutokea eneo la chini ya koromeo la chakula, huleta dalili kama kiungulia, maumivu ya kifua na kushindwa kumeza chakula vizuri.
Nini kinasababisha Ngiri?
Ngiri inasababishwa na kulegea kwa misuli na kupelekea nyama za kiungo kimoja kuota na kusukuma ukuta kuelekea eneo lingine. Kutokana na chanzo cha hernia inaweza kuchukua muda mrefu sana kusambaa na kuleta madhara.
Baadhi ya changamoto zinazopelekea kulegea kwa misuli na hatimaye kuleta ngiri ni pamoja na
- kuzeeka
- matatizo ya kimaumbile kwa mtoto aliyezaliwa
- majeraha kutokana na ajali au upasuaji
- kikohozi sugu
- mazoezi magumu ya kunyanyua vitu vizito
- uzito mkubwa na kitambi
- kuwa na ujauzito wa zaidi ya mtoto mmoja
- kukosa choo na kupata choo kigumu kwa muda mrefu
Makundi gani yapo kwenye hatari zaidi ya kuugua ngiri au hernia?
Makundi yafuatayo yapo kwenye hatari zaidi ya kuugua ngiri kulinganisha na watu wengine
- wajawazito
- wazee
- wanaovuta sigara
- wagonjwa wengi uvimbe tumboni na
- watoto waliozaliwa na uzito dogo ama walizaliwa kabla ya muda
Vipimo Kugundua uwepo wa hernia
Kwa daktari kujua uwepo wa tatizo, atafanya vipimo vya kawaida kutumia mikono yake kwa kushika nyeti zako kuona kama kuna uvimbe au nyama isiyo ya kawaida.
Daktari atachukua historia ya afya yako. Jiandae kwa maswali haya daktari atakayokuuliza hospitali
- lini umeanza kuona uvimbe kwenye sehemu zako za siri?
- unapata dalili gani zingine?
- unafikiri kuna kitu chochote kilichosababisha tatizo kwa upande wako?
- nieleze kuhusu historia ya maisha yako, je unafanya mazoezi magumu kama kunanyua vyuma, na kuvuta sigara?
- je kuna mtu kwenye familia yenu aliyewahi kuugua ngiri?
- umewahi kufanyiwa upasuaji wowote hapo awali?
Daktari pia atahitaji kufanya vipimo Kama CT scan, MRI na utrasound ya tumbo kupata picha ya ndani ili kujua ukubwa wa tatizo.
Endapo utagundulika una hernia ya kifuani(hiatal hernia) basi daktari anaweza kupendekeza ufanyiwe vipimo vingine zaidi kama
Barium X-ray-ambapo unameza kimiminika kisha daktari anapiga picha nyingi kwenye mfumo wa chakula kuonnesha kama kuna michubuko au uvimbe wowote ndani.
Endoscopy– Kifaa chenye camera ndogo kinaingizwa kwa njia ya mdomo, kisha kamera inachukua picha nyingi kuanzia mdomoni mpaka tumboni. Picha hizi zitasaidia kujua ukubwa wa tatizo.
Upasuaji kutibu Ngiri
Endapo ngiri yako imekua kubwa kupita kiasi na imeanza kusambaa na kusababisha maumivu makali, daktari atapendekeza ufanyiwe upasuaji haraka. Upasuaji utalenga kurudisha sehemu za kiungo zilizoota kuelekea eneo lisilo sahihi kisha kushona eneo la tumbo lililolegea mpaka kuruhusu nyama za kiungo kingine kuota.
Upasuaji pia unaweza kufanyikwa kwa njia ya laparascopy. Yaani matundu machache yanatobolewa eneo la tumbo, kisha kifaa chenye kamera kinaingizwa kwenye tundu moja, na kifaa chenye nyembe na sindano za upasuaji kuingizwa katika tundu lingine.
Kuuguza Mshono mpaka kupona baada ya upasuaji
Baada ya upasuaji unaweza kupata maumivu kwenye eneo la mshono. Daktari anayehusika na upasuaji atakupatia dawa za kutumia ili kupunguza maumivu haya wakati unaendelea kujiuguza.
Hakikisha unafatilia kwa makini ushauri aliokupa daktari katika kujiuguza ili uwahi kupona. Rudi hospitali haraka endapo utaona mabadiliko yoyote mabaya kwenye kidonda, mfano maambukizi kwenye kidonda,maumivu kuzidi, homa kali na kidonda kuwa chekundu sana.
Wakati unajiuguza unaweza kushindwa kutembea vizuri na kufanya kazi zako kwa wiki kadhaa. Utahitaji kuepuka kazi zozote ngumu wakati huu. Usinyanyue vitu vizito zaidi ya kilo tano.
Aina za Ngiri
Kuna aina kuu 4 za ngiri. Hapa chini tutaelezea aina hizi kwa kina
1.Mshipa wa ngiri(inguinal hernia)
Ngiri hii ni marufu sana na inawapata watu wengi zaidi. inatokea pale utumbo unaposukuma ukuta unaotenganisha tumbo na via vya uzazi na kuanza kuota mpaka kwenye via vya uzazi. Aina hii ya ngiri inawapata zaidi wanaume.
2.Hiatal hernia(ngiri ya kifuani)
Ngiri ya kifuani inatokea pale sehemu ya tumbo inapovimba na kusukuma ukuta unaotenganisha kifua na tumbo(diaphragm). Ukuta huu wa diphragm unakusaidia wakati wa kuhema kutoa hewa nje na kuvuta hewa ndani ya mapafu. Aina hii ya ngiri inawapata zaidi wazee kuanzia miaka 50 na kuendelea.
Endapo ikitokea kwa mtoto inakuwa imesababishwa na matatizo ya kuzaliwa. Ngiri ya kifuani husababisha kiungulia, yaani chakula cha tumbo kupanda juu mpaka mdomoni na kusababisha hali ya kuunguza kwenye koo.
Umblical hernia(ngiri ya kitovuni)
Ngiri ya kitovuni inawapata zaidi watoto wadogo. Hii inatokea baada ya sehemu ya utumbo kuota kuelekea kwenye kitovu. Utagundua ngiri hii kwa mtoto utakapoona kitovu kinavimba na kuongezeka na mtoto anapolia.
Hii aina pekee ya ngiri ambayo yaweza kuisha yenyewe kadiri misuli ya tumbo inavyokomaa, hasa mtoto akifikisha umri wa miaka miwili. Endapo haitaisha mpaka miaka mitano, upasuaji utahitajika.
Watu wazima pia wanaweza kuugua ngiri ya kitovu, kutokana na kusukumwa mara kwa mara kwa kitovu na vitu kama kitambi, ujauzito na majimaji tumboni.
Incisional hernia
Aina hii ya ngiri hujitokeza kwenye eneo la tumbo lililofanyiwa upasuaji. Pale tishu za mwili zinapoota na kusukuma kuelekea kwenye eneo la upasuaji. Inatokea kutokana na kulegea kwa eneo la mshono.
Nini cha kufanya Kupunguza Maumivu ya Ngiri
Japo huwezi kupona kwa kujitibia nyumbani, lakini kuna baadhi ya mambo unaweza kufanya kupunguza maumivu ya ngiri ukiwa nyumbani.
Ongeza kula vyakula vyenye kambakamba ili upate choo vizuri, usitumie nguvu kubwa unapoenda haja kubwa. Vyakula vya kambakamba ni vile ambavyo havijakobolewa, kama nafaka, matunda, na mboga za majani.
Kama una ngiri ya kifuani, usile mlo mkubwa kwa mara moja, kula kidogo kidogo. Na wakati wa kulala, weka mto eneo la kichwa liwe juu kidogo ili usipate kiungulia. Usitumie vyakula kama pilipili na nyanya. Pia usivute sigara
Ngiri wakati wa ujauzito.
Kama una ngiri na tayari una ujauzito, hakikisha unamuona daktari mapema. Dakari atafanya upembuzi kuona kama tatizo linaleta madhara yoyote kwa mimba uliyobeba.
Kwa kiasi kikubwa upasuaji kwa hernia endapo una mimba hausubiri mpaka siku ya kujifungua. Japo kama mimba bado ni ndogo na ngiri yako inaanza kukua kwa kasi na kukuletea shida zaidi, unaweza kufanyiwa upasuaji wakati huo wa mimba.
Kama uliwahi kuugua ngiri kabla ya ujauzito, kuna hatari ukapata tena ngiri ukishabeba mimba, kwasababu mimba inaleta mgandamizo kwenye viungo vingine vya karibu.
Ngiri pia yaweza kujitokeza baada ya kujifungua kwa upasuaji(cesarian section) kwa tishu za tumbo kukua kuelekea kwenye eneo la mshono.
Madhara ya Ngiri isipotibiwa Haraka
Wakati mwingine ngiri isipotibiwa mapema yaweza kusababisha matizo makubwa. Ngiri yako inaweza kusababisha mgandamizo mkubwa kwenye viungo vya karibu.
Baadhi ya eneo la utumbo wako linaweza kujishikiza kwenye via vya uzazi na kusababisha matatizo makubwa ya choo, na dalili mbaya kama kutapika, kichefuchefu..
Endapo utanona dalili hizi na tayari una ngiri nenda hospitali haraka sana
- Uvimbe unaobadilika rangi
- Maumivu yanayozidi kila mara
- Kichefuchefu na kutapika
- Homa kali na
- Kushindwa kutoa ushuzi ana choo.
9 replies on “Aina za Ngiri na Matibabu”
ugonjwa wa ngiri(henia) unasumbua sana hasa wanaume,tunaomba ushauri mara kwa mara juu ya tatizo hili kabla halijaathiri watu wengi sana asante.
Asantet kwa maelezo mazur
endelea kufatilia makala zetu
asanteni sana mimi nina ngiri na imeshakua na inauma sana wakati mwingine kichefuchefu
Unatakiwa kuwahi hospital haraka ili ufanyiwe upasuaji
Mimi ngili imenianza tangu nikiwa mdogo sana mpaka sasa nina miaka 20 wazaz wangu kula siku wananipeleka kwa waganga wakienyej lakin hakuna dalili zozote za kupona ugujwa huu nifanyaje
usiende kwa mganga wa kienyeji, nenda hospital
Kilichonifurahisha ni hiki “hatuna dawa nenda hospitali ukatibiwe”. Hamko kibiashara bali kuelimisha na kuhudumia. Good.
Naomba kujua dawaza asili zakutibu ngiri