Kipimo cha CT scan ni kifupi cha maneno computerized tomography scan. Ni kipimo kinachotumia mionzi yaani X rays na computer kutengeneza picha ya eneo la mwili. Picha hizi zinapotafsiriwa na daktari, zinatoa mwanga juu ya tatizo lina lokusumbua. CT scan inaweza kutoa picha za tishu laini za miwli, mirija ya damu na hata sehemu za mifupa.
Viungo vingine ambapo CTscan yaweza kutumika kuchunguza ni pamoja na
- kichwa
- mabega
- uti wa mgongo
- tumbo
- magoti
- kifua
Nini kinapelekea ufanyiwe kipimo cha CT scan?
CT scan inatumika zaidi kufanya upimaji wa ugonjwa unaokusumbua pamoja na kucheki eneo lililopata ajali ndani ya mwili. Picha zinazotolewa kwenye kipimo, zitamsaidia daktari
- kujua uwepo wa maambukizi, magonjwa ya misuli na mfupa uliovunjika
- kutambua eneo hasa lenye uvimbe ikiwemo uvimbe wa saratani
- kupima mirija ya damu na viungo vingine vya ndani ya mwili
- kupima ukubwa wa athari ya ajali na damu iliyovuja ndani ya mwili
- kumwongoza daktari katika kufanya upasuaji na kuchukua sampuli (biopsies)
- kufatilia ufanisi wa tiba fulani, ikiwemo tiba ya saratani na magonjwa ya moyo.
Jinsi gani kipimo cha CT scan kinafanyika
Daktari atakupatia kimiminika kinaiwa dye. Kimiminika hicho kinasaidia kuongeza ufanisi wa kipimo, kwa kutoa picha zenye ubora wa hali ya juu, na pia kufanya viungo vya mwili kuonekana vizuri.
Kwa kulingana na aina ya kipimo, daktari anaweza kukwambia unywe kimiminika hiki. Pia daktari anaweza kukuchoma sindano kwenye mkono ili kuingiza kimiminika hiki ama kungiza dawa kupitia njia ya haja kubwa. Daktari atakushauri ufunge kula kwa muda wa masaa manne mpaka sita kabla ya kufanyiwa kipimo.
Wakati wa kipimo
Wakati wa kipimo, utaambiwa ubadili mavazi na kuvaa gauni la hospitali na pia kuvua vitu vyote vya chuma ulivyovaa. Vitu vya chuma vinaweza kuingilia ufanisi wa vipimo. Vifaa hivi ni kama saa, pete, mkufu , mkanda nk.
Daktari atakuomba ulale chali kwenye meza ambayo itasukumwa na kuingizwa ndani ya kipimo. Wakati kipimo kinapita na kuchukua picha, utaweza kuwasiliana na madaktari moja kwa moja.
Wakati unaingiwa kwenye chombo mfano wa bomba kubwa, mashine ya X ray itazunguka na kuchukua picha nyingi za mwili. Mlolongo mzima wa kupimwa unachukua kama dakika 20 mpaka lisaa kukamilika.
Mambo ya kuzingatia ukiwa kwenye kipimo
Ni muhimu sana kulala chali na kutulia wakati wa kipimo. Kutingishika kunapoteza ubora wa picha na hivo kupunguza ufanisi wa picha. Daktari atakushauri kubana pumzi ili kuzuia kifua kutanuka na kusinyaa. Endapo anayefanyiwa kipimo ni mtoto, basi daktari ataendekeza mtoto afungwe vizuri kabla ya kumwingiza kwenye mashine.
Baada ya kipimo cha CT scan
Baada ya kipimo, picha zitaumwa kwa mtaalamu wa mionzi avifanyiwe upembuzi zaidi. Kisha daktari atarudi kwako kukupa majibu ya vipimo na tiba nayotakiwa kuipata.
Je kuna hatari yoyote kufanya CT scan?
Kuna madhara kidogo sana ya kufanyiwa CT scan. Unapofanya CT scan, eneo kubwa la mwili linapigwa na mionzi ukilinganisha ma kipimo cha X ray ya kawaida. Pamoja na hilo bado madhara ya kutokana na mionzi ni mdogo sana endapo umepigwa mara moja tu. Hatari ya kupata kansa kutokana na mionzi inaongezeka kwa watoto, hasa kwa mionzi ya kifuani na kwenye tumbo.
Baadhi ya watu wana aleji na kimiminika cha kumeza kabla ya kipimo. Kimiminika kina madini ya iodine yanayoweza kuleta mpambano ndani ya mwili. Hakikisha unamweleza daktari endapo una aleji ya iodine. Daktari anaweza kukupa dawa za aleji ili kupunguza tatizo wakati wa kipimo.
Ni muhimu pia kumweleza daktari endapo una ujauzito. Japo mionzi ya CT scan inaweza isimuathiri mtoto, lakini daktari anaweza kupendekeza kipimo kingne salama zaidi mfano utrasound au MRI kupunguza hatari.