Vidonda mdomoni ni tatizo kubwa linaloathiri watu wengi sana katika maisha ya kawaida. Vidonda hivi vinaweza kutokea aneo lolote la mdomo, kwenye ukuta wa juu, chini ya ulimi, pembeni kwenye mashavu na hata kwenye ulimi wenyewe. Unaweza pia kupata vidonda kwenye koo la chakula. Fahamu pia kwamba kwenye mdomo kuna bakteria wazuri na wabaya. Bakteria wazuri ni kinga dhidi ya bakteria wabaya.
Vidonda vya mdomo kwa kiasi kikubwa siyo tatizo, maana vinatokea na kuisha vyenyewe ndani ya siku kadhaa. Katika mazingira fulani vidonda inaweza kuwa kiashiria cha tatizo kubwa mfano saratani ama maambukizi ya virusi au bakteria.
Changamoto zinazosababisha vidonda mdomoni
Chanzo halili cha vidonda mdomoni inatofautiana kwa kila mtu. Baadhi ya sababu ni hizi
- kuacha kuvuta sigara hivi karibuni
- kula matunda yenye uchachu
- kun’gata ulimi
- kuvaa meno bandia au vyuma vya kupanga meno
- msongo wa mawazo na wasiwasi
- mabadiliko ya homoni wakati wa ujauzito, kubalehe na menopause
- dawa mfano za presha na za kutuliza maumivu
- kuugua magonjwa kama kisukari na magonjwa ya tumbo
Je vidonda mdomoni ni kiashiria cha saratani?
Saratani ya mdomo na vidonda mdomoni ni changamoto mbili zinazotofautiana kwenye dalili zake. Japo saratani huanza kwa vidonda visivyopona. Hapa chini ni tofati kati ya saratani ya modno na vidonda vya mdomo
- vidonda mdomoni huuma wakati saratani haiumi
- vidonda mdomoni vinaisha ndani ya wiki mbili , wakati saratani huendelea kusambaa
- magamba ya vidonda vya saratani yanakuwa magumu, na hayatoki kirahisi
- vidonda vya saratani mara nyingi huwa na mchanganyiko wa weupe na wekundu.
- saratani ya mdomoni hasa huwapata wanaokunywa pombe kupita kiasi na watumia tumbaku
Tiba ya vidonda mdomoni
Kwa kiasi kikubwa vidonda vya mdomo huanza kupungua vyenyewe na kuisha ndani ya siku chache, bila hata ya kutumia dawa. Kwa watu wanaopata vidonda mdomoni mara kwa mara, muhimu kumuona daktari bingwa wa meno, atakupatia dawa za kupunguza tatizo.
Pia daktari wa meno anaweza kukupatia dawa ya kusukutua kuua bakteria wabaya kwenye meno na pia kupunguza ukubwa wa tatizo.
Jinsi ya kujikinga usipate vidonda mdomoni na kuimarisha afya ya mdomo
Japo ni ngumu kuepuka kwa asilimia mia vidonda mdomoni, kuna baadhi ya vitu unaweza kufanya kupunguza ukali wa tatizo na kuzuia vidonda kutokea mara kwa mara.
Njia hizi za kujikinga na tatizo pamoja na kuimarisha mazingira ya mdomo kiujumla ni pamoja na
1.Weka ratiba nzuri ya kusafisha mdomo
Japo kusafisha mdomo kupita kiasi siyo nzuri kwani inaondoa bakteria wazuri, usafi wa mdomo ni muhimu. Baadhi ya dawa za kusafisha meno na mouthwash zinaondoa bakteria wazuri mdomoni na kuchangia kuharibu mazingira ya mdomo. Safisha mdomo mara mbili kwa siku, asubuhi na usiku kabla ya kulala. Tumia dawa asili ya kusafisha meno isiyo na kemikali hatarishi.
2.Kula lishe nzuri yenye virutubishi vya kutosha
Lishe zetu ni chanzo kikubwa cha matatizo ya mdomo ikiwemo vidonda vya mdomo, kuoza meno na hata kunuka mdomo. Ulaji wa chakula sahihi unaimarisha mazingira na kinga ya mdomo. Baadhi ya vyakula vinalinda na kuimarisha bakteria wazuri mdomoni, na vyakula vingine vinaua bakteria hawa.
Vyakula vya kupendelea kula ni vile visivyo na utindikali, vya kusafisha mwili na pia vyenye viambata vinavyozuia kuvimba kwa mwili. Vyakula hivi ni pamoja na
- mboga za majani za kijani
- zabibu na machungwa yenye uchachu kama machungwa
- mboga jamii ya kabeji kama kabeji, broccoili na cauliflower
- nyama, kuku na mayai ya kienyeji
- vyakula vya mafuta mazuri kama mafuta ya kula ya nazi, karanga,parachichi na korosho
- maziwa asili ya mtindi
- vyakula kama vitunguu maji na vitunguu saumu na maepo.
- kunywa maji ya kutosha, green tea na kahawa kiasi kidogo
Muhimu kuepuka matumizi ya vyakula na vinywaji vya sukari, pamoja na vyakula vya makopo. Baadhi ya bakteria wabaya wanaleta vidonda na harufu mbaya mdomoni, sukari ni mbolea kwa bakteria hawa wabaya.
3.Anza kufikiria afya ya mdomo kama afya ya mwili kiujumla
Pengine yaweza kukushangaza kwamba kuna uhusiano kati ya kutofanya mazoezi, msongo wa mawazo, lishe na afya mbovu ya mdomo. Msongo mkubwa wa mawazo unapelekea kupungua kwa mate mdomoni.
Mabadiliko ya mate mdomoni yanachangia kwa kiasi kikubwa ni jinsi gani meno yanajengeka. Pia kupungua kwa mate mdomoni kunachangia kubadili mazingira ya mdomo na hatimaye kuleta vidonda na harufu mbaya mdomoni.
Kupambana na msongo wa mawazo na kujiwekea ratiba ya kufanya mazoezi ni hatua muhimu katika kurekebisha mazingira ya mdomo. Mazoezi pia ni mazuri sana kuchochea utoaji wa sumu mwilini, na hivo kuimarisha afya ya meno, ulimi na fizi.
Lini unatakiwa kumwona daktari?
Muone daktari mapama endapo
- unapata vidonda vingi mdomoni vilivyoleta maumivu
- kidonda kisicho cha kawaida kimejitokeza
- vidonda vinamsambaa
- vidonda haviishi hata baada ya wiki tatu
- mumivu makali sana yasiyovumilika
- kidonda kimevimba sana na ni kikubwa
- vidonda vinaambatana na homa kali
- umepata vidonda baada ya kutumia dawa fulani
Pia muone daktari endapo dawa alizokupatia zimesababisha vidonda. Daktari atakucheki, kisha atakubadilisia dawa.