Ni umri gani tunasema umeshika mimba uzeeni?
Kuanzia miaka 35 tunasema ni umri mkubwa zaidi wa kushika mimba (advanced martenal age)
Kutokana na sababu mbalimbali, wanawake wanaweza kuamua kuchelewa sana kutafuta mtoto. Hii imekuwa tabia maarufu sana katika miaka ya hivi karibuni. Mabadiliko ya teknologia yamechangia sana. Mfano mtu anaweza kuamua kutunza mayai na mbegu kisha zikatumika hata baada ya miaka mi5 kushika mimba.
Pamoja na teknologia kukua, bado hatari ya kubeba mimba katika umri mkubwa ipo. Changamoto kama mimba kuharibika, kifafa cha mimba, kujifungua kwa upasuaji nk
Kwanini ni hatari kubeba mimba katika umri mkubwa?
Kadiri umri unavosogea, uwezekano wa kuugua magonjwa sugu unaongezeka. Magonjwa kama kisukari, presha ya kupanda na magonjwa ya tezi ya shingo. Hata kama afya yako iko njema kabla ya mimba, unapopata mimba italeta mabadliko ya kukuweka kwenye changamoto.
Wanawake wanaobeba mimba katika umri zaidi ya 35 wapo kwenye hatari ya
- mimba kutunga nje ya kizazi
- mimba kutoka mapema
- kuchelewa kujifungua
- matatizo ya kondo la nyuma
- kisukari cha mimba
- presha ya kupanda
- kifafa cha mimba
- kujifungua mapema kabla ya wakati
- kupungukiwa damu
- magonjwa ya moyo
- kuziba mishipa ya damu
- kuvuja damu nyingi baada ya kuzaa
Changamoto kwa mtoto
Kuna ongezekeno la hatari ya mamatizo ya hitilafu za vinasaba, pale mayai yanapozeeka. Mwanaume yeye anazalisha mbegu mpya kila siku, ila kwa mwanamke ni tofauti.
Mwanamke anazaliwa na mayai yote, hakuna mayai mapya yanayozalishwa tena, ila tu yanapevuka kila mwezi. Mayai haya yanavokaa miaka mingi yanazeeka na kuwa na hitilafu za kivinasaba.
Kwa mtu mzima, mzunguko wa damu kwenye via vya uzazi na kuelekea kwenye kondo la nyuma unapungua, na hivo kupelekea ukuaji hafifu wa mtoto tumboni.
Pia hatari ya kuumwa kwa mjamzito katika umri mkubwa inaongeeka, na kuathiri ukuaji wa mtoto, kupungua majimaji ya mtoto, na kujifungua njiti.
Maandalizi ya kubeba mimba katika umri mkubwa
Wataalamu wa uzazi wanashauri kuweka sawa uzito wako, kufanya mazoezi, kula vizuri na kupunguza stress ni muhimu pale unapotaka kubeba mimba katika miaka 35+
Muone daktari akufanyie vipimo hasa kwa magonjwa ya kisukari, tezi ya shingoni, na presha ya kupanda. Ni muhimu sana kupima magonjwa haya kabla hujashika mimba kwasababu yanaweza kuwepo bila dalili yoyote. Hakikisha unamweleza daktari anayekupima kwamba unajaribu kubeba mimba.
Je mama mtu mzima atapata changamoto gani kwenye kujifungua?
Mjamzito anapokaribia kujifungua, kondo la nyuma huanza kulegea. Hii inamaanisha mishipa ya damu inaanza kuzeeka, na usafirishaji wa chakula na hewa kuelekea kwenye mtoto unapungua. Lengo ni kumuandaa mtoto kuanza kujitegemea kula akitoka nje ya tumbo.
Kitendo hichi kinatokea mapema sana kwa wajawazito wa umri mkubwa. Yaani usafirishaji unapungua mapema kabla ya muda muafaka wa kujifungua. Ndiomaana katika umri huu, mimba ikifika tu wiki 39 na hujapata uchungu, unazalishwa kwa lazima ili kumuokoa mtoto.
Watu wazima wako kwenye uwezekano mkubwa wa kujifungua kwa upasuaji kwasababu wanakosa nguvu ya kusukuma mtoto. Na watoto wanaozaliwa na wazazi wazee, wanaweza kuwa mapigo ya moyo ya tofauti na hivo kujifungua kwa njia ya uke ikawa hatari kwao.